• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 1:13 PM
JAMVI: Je, ni busara kwa Kalonzo kuungana na Jubilee?

JAMVI: Je, ni busara kwa Kalonzo kuungana na Jubilee?

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka ameanza kucheza kamari ya kisiasa kwa njia tofauti, akitangulia na kuondoa chama chake kwenye muungano wa National Super Alliance (NASA) na kukiunganisha na chama tawala cha Jubilee.

Wadadisi wa siasa wanasema ni hatua inayoweza kudumisha nyota yake ya kisiasa iking’aa au kuwa pigo kwa maisha yake ya kisiasa.

Mnamo Jumanne, Baraza Kuu la Kitaifa la Wiper (NEC) lilipitisha kwamba chama hicho kijiondoe katika muungano wa NASA ambao pia unashirikisha vyama vya ODM chini ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, Amani National Congress (ANC) chini ya Musalia Mudavadi, Ford Kenya cha Moses Wetangula na Chama cha Mashinani (CCM) cha aliyekuwa gavana wa Bomet, Bw Isaac Ruto.

Kulingana na taarifa ya Katibu Mkuu, Bi Judith Sijeny, Wiper iliamua kuungana rasmi na Jubilee kwa sababu NASA imekufa.

Hata hivyo, katika kile ambacho wadadisi wanasema ni makosa makubwa katika kamari ya kisiasa, vyama vingine katika NASA vimekosoa uamuzi wa Bw Musyoka na kumtaja kama ndumakuwili.

Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna, mwenzake wa Ford Kenya, Bw Eseli Simiyu na mbunge wa Lugari Ayub Savula wa ANC, walisema wabunge wa Wiper wanafaa kuacha nyadhifa wanazoshikilia bungeni zilizotengewa upinzani.

Kulingana na mdadisi wa siasa Jared Omukwa, Musyoka huenda akashangaa kwa kufikiri atakuwa salama akiungana na Jubilee.

Anasema Musyoka amegundua Bw Odinga hangemuunga mkono kugombea urais.

“Amegundua kwamba hawezi kupata tiketi ya NASA kugombea urais kwa sababu Raila Odinga ameonyesha dalili za kujipanga kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na kwa hivyo hataweza kumuunga mkono.

“Anafikiri kuwa Rais Uhuru Kenyatta atamuunga mkono akiungana naye katika muda wa miaka miwili ambao umesalia amalize kipindi chake cha pili uongozini.Ninachojua ni kwamba itakuwa vigumu Rais Kenyatta kumuunga mkono Bw Musyoka kuwa mrithi wake,”asema Bw Omukwa.

Anasema Bw Odinga ana ukuruba mkuu wa kisiasa na Rais Kenyatta sawa na viongozi wengine wanaomezea mate kiti chake atakapoondoka mamlakani. Mdadisi huyo anasema inawezekana makamu huyo rais wa zamani anajiandaa kuwa katika serikali ijayo chini ya mpangilio mpya wa serikali utakaotokana na mchakato wa kubadilisha katiba (BBI).

“Inafaa kufahamika kuwa ushawishi wake katika ngome yake ya Ukambani unaendelea kufifia baada ya kutofautiana na wandani wake wa muda mrefu kama aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama ambaye ametangaza kuwa atakuwa na chama chake kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Kwa kuungana na Rais Kenyatta, anataka kuokoa nyota yake ya kisiasa kwa kuwa mashinani kunaendelea kuharibika na umaarufu wa chama chake Ukambani unafifia,” asema.

Hata hivyo, wadadisi wanasema anaweza kupata pigo kubwa Rais Kenyatta akimchezea shere na kumuacha kwenye mataa.

“Uamuzi wa Musyoka kuacha NASA na kukumbatia Jubilee haukuwa wa busara kwa sababu Rais Kenyatta si wa kuaminika. Ulifanywa kwa pupa na unaweza kuathiri maisha ya kisiasa ya Bw Musyoka kitaifa na katika eneo la Ukambani,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Mnamo Ijumaa, wakati baadhi ya viongozi wa ODM, ANC na Ford Kenya walipokuwa wakimkashifu kwa uamuzi wa kuhama NASA, Bw Musyoka alikuwa akikutana na Waziri wa Ugatuzi, Bw Eugene Wamalwa na Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya katika kile kinachokisiwa kuwa juhudi za kupanua ukuruba wake na viongozi wa eneo la Magharibi.

Mabw Wamalwa na Oparanya wamekuwa wakipigia debe BBI eneo la Magharibi na ingawa yaliyojiri katika mkutano wao na Bw Musyoka hayakubainika, duru zinasema kiongozi huyo wa Wiper anataka kutafuta miungano mipana ya kisiasa.

Bw Oparanya ambaye ni Naibu Kiongozi wa ODM, ametangaza azma ya kugombea urais. Wadadisi wanasema kwa kumshawishi Oparanya, Bw Musyoka anachimba maji kwenye mawe ikizingatiwa gavana huyo ni mwandani wa Bw Odinga na hawezi kugombea urais iwapo waziri huyo mkuu wa zamani atakuwa kwenye debe.

Duru katika chama cha Wiper zinasema uamuzi wa kuhama NASA haukuwafurahisha wabunge wa Wiper ambao wanahisi kwamba watapoteza nyadhifa zao.

Kulingana na Bi Sijeny, chama hicho kiko tayari kupoteza nyadhifa hizo na kimewahakikishia wabunge watakaoathiriwa kwamba watapata nyadhifa nyingine wakiwa upande wa serikali.

Hata hivyo, wadadisi wanasema tayari nafasi za uongozi bungeni zimegawanywa na itakuwa vigumu mabadiliko kufanywa wakati huu.

Mbunge mmoja wa Wiper ambaye hakutaka tutaje jina alisema wengi wao walilamika kwamba uamuzi wa kuungana na Jubilee haukufaa kwa wakati huu lakini hawakufaulu kushawishi viongozi wa chama.

“Hii itaathiri umaarufu wa Musyoka mashinani kwa sababu wabunge wanahisi anaongozwa na ubinafsi tu,” alisema

You can share this post!

Binti akasirisha baba kwa kuamua kumpinga kisiasa

Sonko azomewa kwa kudai kuwa alileweshwa Ikulu

adminleo