• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Jamie Vardy aibuka mfungaji bora mkongwe zaidi katika EPL

Jamie Vardy aibuka mfungaji bora mkongwe zaidi katika EPL

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI wa Leicester City, Jamie Vardy aliweka rekodi ya kuwa mwanasoka mkongwe zaidi kuwahi kutwaa taji la Mfungaji Bora katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kukamilisha rasmi kampeni za msimu huu kwa mabao 23.

Nyota huyo aliye na umri wa miaka 33, alimzidi Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal na Danny Ings wa Southampton waliopachika wavuni mabao 22 kila mmoja katika msimu wa 2019-20.

Vardy ndiye mwanasoka wa tisa mzawa wa Uingereza kuwahi kuibuka mfungaji bora wa EPL na hivyo kutwaa kiatu cha dhahabu.

Msimu uliopita wa 2018-19, wanasoka wawili wa Liverpool yaani Sadio Mane na Mohamed Salah pamoja na Aubameyang wa Arsenal waliibuka wafungaji bora baada ya kila mmoja wao kupachika wavuni mabao 22.

Vardy alitawazwa mfungaji bora licha ya kikosi chake cha Leicester kupokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Manchester United katika siku ya mwisho ya kampeni za muhula huu uwanjani King Power mnamo Julai 26, 2020.

Ushindi kwa Man-United uliwapa tiketi ya kurejea katika kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao huku Leicester wakilazimika sasa kujiandaa kwa kivumbi cha Europa League baada ya kutupwa hadi nafasi ya tano kwa alama 62, nne nyuma ya Chelsea waliotoshana alama na Man-United walioambulia nafasi ya tatu.

Vardy alifunga mabao zaidi katika msimu wa 2015-16 uliowashuhudia Leicester wakiibuka mabingwa wa taji la EPL. Wakati huo, mfumaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, alifunga mabao 24, moja nyuma ya Harry Kane wa Tottenham Hotspur aliyetia kapuni kiatu cha dhahabu.

Ederson Moraes wa Manchester City alimpiku mlinda-lango Nick Pope wa Burnley na hivyo kuibuka Kipa Bora wa EPL msimu huu. Ederson aliwaongoza waajiri wake Man-City kuwapepeta Norwich City 5-0 katika mchuano wa 16 alioukamilisha bila ya kufungwa bao.

Pope kwa upande wake alifunga bao moja katika ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Brighton dhidi ya Burnley mnamo Julai 26, 2020.

You can share this post!

Juventus wanyakua taji la Serie A kwa msimu wa tisa...

Babu Owino sasa ni mfano tosha wa ‘mui huwa...

adminleo