Inter waruka Atalanta, waikaribia Juve
Na CHRIS ADUNGO
INTER Milan walipaa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na kupunguza pengo la alama kati yao na Juventus hadi pointi nne pekee baada ya kuwapepeta Genoa 3-0 mnamo Jumamosi.
Mabao yote ya Inter ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte yalijazwa kimiani na wanasoka Romelu Lukaku na Alexis Sanchez.
Juventus wanaopigiwa upatu wa kutwaa ubingwa wa taji la Serie A msimu huu, walikuwa jana wageni wa Sampdoria. Hadi waliposhuka dimbani, masogora hao wa kocha Maurizio Sarri walikuwa wamesajili ushindi mara moja pekee kutokana na mechi tano za awali.
Lukaku aliwafungulia Inter ukurasa wa mabao kunako dakika ya 34 baada ya kukamilisha krosi ya Cristiano Biraghi kwa ustadi mkubwa. Alifunga bao lake la pili na la tatu kwa upande wa Inter mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya Sanchez kucheka na nyavu katika dakika ya 82.
Ushindi kwa Inter uliwawezesha kuwaruka Atalanta ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 75, moja nyuma ya Inter. Genoa kwa upande wao wananing’inia padogo mkiani mwa jedwali kwa alama 36, nne zaidi kuliko Lecce ambao kwa pamoja na Brescia na Spal, wako katika hatari ya kuteremshwa daraja mwishoni mwa muhula huu.
Sanchez na beki Chris Smalling wa Manchester United walirefusha vipindi vyao vya mkopo kambini mwa Inter na AS Roma mtawalia hadi mwishoni mwa kampeni za msimu huu katika soka ya Serie A.
Smalling ambaye ni beki mzawa wa Uingereza na Sanchez ambaye ni fowadi raia wa Chile, wamekuwa wakinogesha kivumbi cha Serie A tangu Agosti 2019.
Walitarajiwa kurejea uwanjani Old Trafford, Uingereza mnamo Juni 30, 2020 baada ya mikataba yao katika soka ya Italia kutamatika. Kipute cha Serie A ambacho kilivurugwa na janga la corona msimu huu kinatarajiwa sasa kukamilika rasmi mnamo Agosti 2, 2020.
Uwezekano wa Smalling na Sanchez kuwa sehemu ya kampeni za klabu zao za sasa katika kampeni za Europa League zitakazorejelewa mnamo Agosti 5, 2020 bado haujathibitishwa.
Klabu zote tatu; yaani Roma, Inter na Man-United zingalipo katika vita vya kuwania ufalme wa Europa League msimu huu. Man-United walitinga robo-fainali baada ya kuwazamisha LASK kutoka Austria kwa mabao 5-0 katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora.
Inter wamepangiwa kuchuana na Getafe huku Roma wakiratibiwa kuvaana na Sevilla kwenye marudiano ya hatua ya 16-bora mnamo Agosti 5-6, 2020 ili kujikatia tiketi za robo-fainali.
Hadi kufikia sasa, Sanchez amechezea Inter wanaoshikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Serie A jumla ya mechi 23. Mbali na Lukaku na Sanchez, Inter wanajivunia pia huduma za mwanasoka wa zamani wa Man-United, Ashley Young.