Michezo

Maddison arefusha mkataba Leicester

July 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO James Maddison wa Leicester City ametia saini mkataba mpya ambao kwa sasa utamshuhudia akipokezwa mshahara wa Sh13 bilioni mwishoni mwa kila wiki hadi mwaka wa 2025.

Kufaulu kwa mpango huo ni pigo kubwa kwa Manchester United waliotarajiwa kumshawishi nyota huyo mzawa wa Uingereza kujiunga nao mwishoni mwa msimu huu.

Maddison hatakuwa sehemu ya kikosi cha Leicester kitakachovaana Manchester United katika mechi ya mwisho ya kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kutokana na jeraha la paja.

Malipo atakayokuwa akipokezwa kwa sasa mwishoni mwa kila juma yanamfanya kuwa miongoni mwa wanasoka wanaodumishwa kwa ujira wa juu zaidi uwanjani King Power. Kufikia sasa, ni mshambuliaji Jamie Vardy anayepigiwa upatu wa kuibuka mfungaji bora wa EPL msimu huu wa 2019-20 ndiye alilipwa mshahara wa juu zaidi kambini mwa Leicester City. Sogora huyo mzawa wa Uingereza hutia mfukoni kima cha Sh16.8 milioni kwa wiki.

Maddison, 23, aliingia katika sajili rasmi ya Leicester mnamo 2018 baada ya kuagana na Norwich City kwa kima cha Sh3 bilioni. Wakati huo, alitia saini mkataba wa miaka mitano.

Chini ya mkufunzi wa zamani wa Liverpool na Celtic, Brendan Rodgers, Leicester wanatazamiwa kufungua rasmi uwanja wao mpya viungani mwa mji wa Seagrave kabla ya kivumbi cha msimu ujao kung’oa nanga.