Nusura Klopp avunje rekodi ya Guardiola
Na CHRIS ADUNGO
MABINGWA Liverpool walikamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa idadi kubwa zaidi ya alama katika historia yao ya kushiriki kivumbi hicho baada ya kutoka nyuma na kuwazamisha Newcastle United 3-1 uwanjani St James’ Park mnamo Julai 26, 2020.
Masogora hao wa kocha Jurgen Klopp walitia kapuni jumla ya alama 99, moja zaidi kuliko zile walizojizolea katika msimu wa 1978-79. Liverpool walidumisha pengo la pointi 18 kati yao na nambari mbili Manchester City waliowaponda Norwich City 5-0 katika mchuano wao wa mwisho wa msimu huu uwanjani Etihad.
Liverpool ambao walijizolea alama 97 mnamo 2018-19, walifikia pia rekodi ya Man-City ambao hadi mwanzoni mwa msimu wa 2019-20, walikuwa wakijivunia kushinda idadi kubwa zaidi ya mechi katika msimu mmoja; yaani 32 katika msimu wa 2017-18 na 2018-19.
Hata hivyo, Liverpool walishindwa kufikia rekodi ya Man-City ambao walikamilisha msimu wa 2017-18 wakijivunia pengo la alama 19 kati yao na nambari mbili Machester United. Man-City walifunga kampeni zao za msimu huo kwa alama 100, mbili kuliko za muhula wa 2018-19.
Nyota Dwight Gayle aliwaweka Newcastle kifua mbele baada ya dakika 25 pekee za ufunguzi wa kipindi cha kwanza baada ya kukamilisha kwa ustadi mpira wa ikabu uliochanjwa na Jonjo Shelvey. Goli hilo lilikuwa la haraka zaidi kuwahi kufungwa katika siku ya mwisho ya kampeni za EPL.
Liverpool walioanza mechi hiyo kwa kuwaweka benchi wavamizi wao watatu wakuu yaani Mohamed Salah, Sadio Mane na Robert Firmino; walisawazishiwa na beki Virgil van Dijk aliyefunga kwa kichwa kunako dakika ya 38.
Divock Origi aliwaweka Liverpool kifua mbele kunako dakika ya 59 baada ya kushirikiana vilivyo na beki Andrew Robertson kisha Mane akazamisha kabisa chombo cha wenyeji wao mwishoni mwa kipindi cha pili