• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
WANGARI: Mbinu za sayansi ni bora katika kulinda wanyama

WANGARI: Mbinu za sayansi ni bora katika kulinda wanyama

Na MARY WANGARI

MAJUZI, Shirika la Kulinda Wanyamapori Nchini (KWS) liliibua hisia kali lilipochapisha kwenye mtandao wa Twitter kuhusu matumizi ya mbinu za upangaji uzazi katika Hifadhi ya Wanyamapori ya Lewa.

Hii si mara ya kwanza kwa KWS kujipata katika hali kama hiyo kutokana na baadhi ya vitendo vyake vinavyoonekana kukinzana na uhifadhi wa wanyamapori na mazingira.

Mnamo 2016, kwa mfano, KWS ilikemewa vikali ilipochukua hatua ya kumpiga risasi simba mla watu aliyemvamia mwendeshaji bodaboda baada ya kutoroka kutoka Mbuga ya Wanyamapori ya Nairobi.

Kisa hicho ni ithibati tosha kuwa wakati umewadia kwa Wakenya kukumbatia sayansi katika usimamizi wa wanyamapori na mazingira badala ya kushikilia hisia zisizo na mashiko na mtazamo wa kijadi hasa miongoni mwa wakereketwa wa haki za wanyama.

Ni kwa kufanya hivi tu ndipo tutaweza kuhifadhi wanyamapori nchini bila kutatiza mpangilio wa maumbile na utangamano baina ya binadamu, wanyama na mimea.

Inatamausha kuona Kenya ikiwa imekwama katika sheria zilizopitwa na wakati zinazozuia taifa kujinufaisha kutokana na urithi wa wanyamapori, huku wanyama hao wakizidi kupungua kutokana na kutatizwa kwa utaratibu wa kimaumbile.

Licha ya data ya kisayansi kuthibitisha haja ya kuwepo mikakati ya usimamizi, KWS imelemazwa huku ikionekana kuhofia kuamsha hasira ya wanaharakati kuhusu haki za wanyamapori, wengi wao wakiwa wanaoungwa mkono na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Kwa kawaida, idadi ya wanyama huongezeka pakubwa nyakati za mvua ambapo kuna lishe nyingi inayotoa mazingira mwafaka kwa wanyama kuzaana.

Endapo idadi fulani ya wanyama itaongezeka kupita kiasi, itatatiza usawa wa kimaumbile hivyo kusababisha madhara katika msururu asilia wa chakula, hali inayojitokeza waziwazi nyakati za kiangazi.

Njia pekee ya kuzuia hali hiyo ni kudhibiti idadi hiyo ya wanyamapori, hatua inayokabiliwa na pingamizi kali kutoka kwa wakereketwa wa haki za wanyama.

Hoja kwamba ni ukatili kudhibiti idadi ya wanyamapori haina mashiko kwa kuwa ni vigumu kupata usawa wa kimaumbile pasipo kuhusisha mchango wa binadamu katika usimamizi.

Ni kinaya kuruhusu idadi ya wanyamapori kuongezeka kupita kiasi pasipo kuwadhibiti kwa kisingizio cha kuwajali na badala yake kushuhudia wakifariki kwa maelfu kutokana na uhaba wa chakula na maradhi yanayotokana na msongamano.

Ikizingatiwa kuwa mbuga na hifadhi za wanyamapori nchini ni ndogo, hivyo hazina uwezo wa kumudu idadi kubwa ya wanyamapori, ni dhahiri kuwa haja ya kuunga mkono mikakati ya usimamizi wa wanyamapori kisayansi haiwezi kusisitizwa kikamilifu.

Iwe ni kwa kutumia mbinu za upangaji uzazi au vinginevyo katika juhudi za kudhibiti wanyamapori, ni sharti tusonge na majira ili kuepuka athari zinazotokana na kuvurugwa kwa mpangilio kimaumbile.

[email protected]

You can share this post!

Huenda wageni kutoka nje wasiende karantini – Balala

COVID-19: Visa vipya ni 606 idadi jumla nchini Kenya...

adminleo