• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
KAMAU: Mkapa alikuza mbegu ya demokrasia Afrika

KAMAU: Mkapa alikuza mbegu ya demokrasia Afrika

Na WANDERI KAMAU

TANZANIA ni miongoni mwa mataifa yenye mifumo thabiti zaidi ya kidemokrasia barani Afrika.

Tangu ijipatie uhuru mnamo 1961 kutoka kwa Uingereza, taifa hilo limeibuka kuwa kati ya mifano ya kuigwa kwenye uendelezaji na uzingatiaji wa demokrasia.

Hatua ya kwanza ambayo inaonekana kuchangia mwelekeo huo mzuri ni msingi wa kiutawala uliowekwa na kiongozi wa kwanza, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Kinyume na viongozi wengine wa kizazi chake barani, Nyerere alianza harakati za kubuni mfumo wa utawala ambapo Tanganyika (Tanzania bara) iliungana na kisiwa cha Zanzibar kuwa jamhuri moja.

Nyerere alifanikiwa kufanya hivyo 1964, hiyo ikiwa hatua ya kwanza kujenga mfumo thabiti wa uongozi ambao umekuwa ukizingatiwa na viongozi wanaochaguliwa kuwa marais wa taifa hilo.

Upeo wa kujitolea kwa Nyerere ulidhihirika 1967, alipozindua rasmi Sera ya Ujamaa ya chama cha Tanganyika African National Union (TANU) chini ya Azimio la Arusha. Hilo liliendelea kuweka msingi thabiti wa kisiasa nchini humo.

Hivyo, alipofariki Ijumaa iliyopita,ilitarajiwa rais wa tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa kusifiwa kama kiongozi aliyechangia sana kwenye juhudi za kukuza demokrasia nchini humo na Afrika kwa jumla.

Juhudi za Mkapa zilionekana na kila mmoja. Wakenya ni miongoni mwa wale waliofaidika pakubwa kutokana na uungwana wake, alipohudumu kama mmoja wa wapatanishi wakuu kwenye mazungumzo ya kutafuta amani kufuatia ghasia baada ya uchaguzi 2007. Sifa za Bw Mkapa hazikuwa za kusingiziwa kama ambavyo imekuwa kawaida kwa viongozi wengine barani wanapofariki.

Baada ya kuhudumu kwa miaka kumi kama rais kati ya 1995 na 2005, aliondoka uongozini kwa hekima na kumpisha mwenzake, Jakaya Kikwete.

Bw Kikwete naye alihudumu kati ya 2005 na 2015 na kunga’atuka wakati wake ulipoisha. Hilo ndilo lililompisha rais wa sasa, John Magufuli.

Bila shaka, Tanzania ndilo taifa la pekee Afrika Mashariki ambalo halijashuhudia ghasia zozote za kisiasa tangu uhuru wake. Halijawahi kukumbwa na migogoro kama jaribio la mapinduzi dhidi ya utawala uliopo. Hili ni kinyume na nchi zingine za eneo la Afrika Mashariki kama Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda na Sudan Kusini.

Ingawa serikali ya Rais Magufuli imekuwa ikilaumiwa kwa kukiuka kanuni hizo mara kwa mara, ni dhahiri bado anazingatia msingi uliowekwa na Mwalimu Nyerere.

Wakati umewadia kwa viongozi nchini kujifunza kutoka kwa Tanzania, kuwa msingi thabiti wa kisiasa huchangia pakubwa kwa ustawi wa taifa husika katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

Hili pia limechangiwa na uwepo wa vyama thabiti vya kisiasa kama Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kati ya vingine.

Anapozikwa leo Jumatano, Mkapa atakumbukwa kama kiongozi muungwana aliyejitolea kuona demokrasia ya kweli ikinawiri katika kila sehemu barani Afrika.

Mola amweke pema pa wema.

[email protected]

You can share this post!

Kikao cha seneti chaahirishwa malumbano yakiwa yamechacha

KINA CHA FIKIRA: Kisa cha Mlajasho mfano kwa vijana

adminleo