Kenya ina PPE za kutosha, asema Kagwe
Na SAMMY WAWERU
KENYA ina vifaa vya kutosha kukinga wahudumu wa afya dhidi ya kuambukizwa Covid-19, imesema Wizara ya Afya.
Waziri katika Wizara Mutahi Kagwe Jumatano amewataka Wakenya kutokuwa na wasiwasi wowote, akisema serikali imehami vituo vya afya kwa vifaa vya kutosha, PPE.
Katika kikao na wanahabari jijini Nairobi wakati akitoa taarifa ya maambukizi ya virusi vya corona nchini chini ya saa 24 zilizopita, Waziri hata hivyo alisema baadhi ya wahudumu wa afya wanapuuza mikakati iliyowekwa kuwazuia kuambukizwa.
“Ninaweka wazi kuwa tuna vifaa vya kutosha (PPE) kukinga wahudumu wetu wa afya kuambukizwa Covid-19. Baadhi ya visa vya maambukizi miongoni mwao tunavyoskia vinajiri kwa sababu ya utepetevu,” Bw Kagwe akasema.
Aidha, alisema kufikia sasa jumla ya wahudumu 634 wamethibitishwa kuambukizwa corona. Waziri alisema idadi hiyo ni ya chini mno, ikilinganishwa na mataifa mengine ulimwenguni.
“Wahudumu wa afya, ninawahimiza mdumishe uadilifu miongoni mwenu. Tunayosema, muyatekeleze. Tuhubiri kunywa maji, na tuyanywe, ila si kufanya mambo kinyume,” Bw Kagwe akasema, akionekana kulenga wahudumu wanaokiuka sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia kusambaa kwa corona.
Waziri alitangaza kwamba chini ya saa 24 zilizopita watu 544 wamethibitishwa kuambukizwa Covid-19, idadi hiyo ikifikisha jumla ya visa 19,125 vya maambukizi yaliyoandikishwa nchini.
Kagwe alihimiza Wakenya kuwajibika na kuepuka kukongamana, huku akiwataka kutii sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia msambao zaidi.
Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, Kenya imethibitisha maafa ya wagonjwa 12 wa corona. Kufikia sasa, idadi ya waliofariki kutokana na Covid-19 imefika 311.
Wakati huohuo, wagonjwa 113 wameruhusiwa kuondoka katika vituo mbalimbali vya afya nchini, baada ya kuthibitishwa kupona kabisa. Takwimu hiyo inafikisha jumla ya 8,021 waliothibitishwa kpona corona nchini.