Michezo

Mikoba ya Shujaa yavutia makocha 11 wa kigeni na watatu wa humu nchini

July 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

JUMLA ya makocha 14 kutoka ughaibuni na humu nchini wamewasilisha maombi ya kupokezwa fursa ya kudhibiti mikoba ya timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Shujaa.

Kati ya 14 hao, 11 ni raia wa kigeni hasa kutoka mataifa ya New Zealand, Australia, Afrika Kusini na Uingereza. Wote hao wanawania nafasi ya kurithi mikoba iliyoachwa na Paul Feeney – raia wa New Zealand aliyeagana rasmi na Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) mnamo Mei 2020.

Japo mchakato wa kutafuta mrithi wa Feeney ulianzishwa na KRU mwezi Juni, shirikisho lilitangaza upya nafasi hiyo ya kazi mnamo Julai baada ya makocha watatu pekee wa humu nchini kuwasilisha maombi.

Lengo lilikuwa ni kutoa fursa kwa wakufunzi wa kigeni kutuma maombi yao ya kazi.

KRU inasaka kocha atakayetambisha wanaraga wa Shujaa kwenye Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan mwakani.

“Tunatafuta kocha kutoka nchi yoyote aliye na tajriba ya kudhibiti mikoba ya kikosi cha haiba kubwa kwa zaidi ya miaka mitatu. Awe amehitimu kiwango cha pili cha ukufunzi (Rugby Level 2 Certificate) katika kikosi cha wanaraga saba au 15 kwa mujibu wa viwango vya Raga ya Dunia,” ikasema taarifa ya KRU.

Thomas Odundo ambaye ni mkurugenzi wa raga wa KRU amethibitisha kwamba waliotuma maombi bado wanahojiwa na orodha fupi ya mwisho itafichuliwa wiki ijayo kabla ya kocha mpya kutambulishwa rasmi kwa kikosi na mashabiki kufikia mwisho wa wiki ya pili ya mwezi Agosti.

“Nia imekuwa kutoa fursa kwa kila mtu. Tunapania kupata kocha bora zaidi ambaye tajriba yake itafufua makali ya Shujaa, kurejesha uthabiti wa kikosi na kukifanya kiwe tishio kwa wapinzani wengine katika majukwaa ya  kimataifa kadri atakavyokuwa akikisuka kwa msimu ujao,” akasema Odundo kwa kusisitiza kwamba huenda wakalazimika kufutilia mbali kampeni za raga ya Ligi Kuu ya Kenya Cup msimu huu wa 2019-20 kwa sababu ya janga la corona.

Kenya imejivunia idadi kubwa ya wakufunzi wa raga katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ambayo imeshuhudia mikoba ya Shujaa ikidhibitiwa na wakufunzi Mitch Ocholla, Mike Friday wa Amerika, Paul Treu wa Afrika Kusini, Felix Ochieng, Innocent Simiyu na Paul Murunga.

Kocha mpya wa Shujaa anatarajiwa kuanza kazi mnamo Oktoba 2020 kwa kibarua cha kuongoza Kenya kuwa mwenyeji wa kipute cha kimataifa cha Safari Sevens.

Feeney ambaye alikuwa kocha wa nne wa kigeni kuwahi kudhibiti mikoba ya Shujaa, alirejea kwao New Zealand baada ya kuongoza timu ya taifa kutia kibindoni ubingwa wa Raga ya Afrika jijini Johanesburg, Afrika Kusini. Ushindi huo uliwakatia Shujaa tiketi ya kufuzu kushiriki makala yajayo ya 32 ya Michezo ya Olimpiki.

Feeney aliyewahi kudhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Fiji mnamo 2015, pia aliiongoza Kenya Morans kutinga fainali ya Tusker Safari Sevens mnamo 2019.

Chini yake, Shujaa walikamilisha kampeni za Raga ya Dunia muhula huu katika nafasi ya 12 katika orodha ya timu 17 baada ya msimu wote kufutiliwa mbali kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19 zikiwa zimesalia duru nne za London, Paris, Singapore na Hong Kong.

New Zealand walitawazwa mabingwa wa Raga ya Dunia msimu huu wa 2019-20 kwa pointi 115. Kenya ilijizolea jumla ya alama 35 ya kutinga robo-fainali za Main Cup mara mbili jijini Cape Town na Hamilton.

Shirikisho la Raga la Dunia (WR) limethibitisha pia kufutilia duru mbili za kwanza za Dubai na Cape Town katika Raga ya Dunia ya 7’s msimu ujao wa 2020-21.