• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
WANGARI: Serikali itumie muda huu kuimarisha taasisi za elimu

WANGARI: Serikali itumie muda huu kuimarisha taasisi za elimu

NA MARY WANGARI

MNAMO Jumatatu, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa, Wizara ya Afya itatoa mwelekeo kuhusu ufunguzi wa shule hivi karibuni.

Ukweli ni kwamba, kuahirishwa kwa kalenda ya masomo 2020 kumezua utata miongoni mwa wazazi na wanafunzi, hususan, watahiniwa wa mitihani ya kitaifa.

Wahudumu na wafanyabiashara wengineo wanaotegemea sekta ya elimu kujipatia riziki wameathirika pakubwa huku uwezekano wa kufungua tena taasisi za elimu ukionekana kuwa mbali kila uchao.

Hatua ya kusitisha mafunzo nchini ina madhara chungu nzima.

Hivyo basi, tunaweza kuamua kuwa na mtazamo chanya na kuangazia palipo na mwanga wa matumaini.

Japo hatua ya kufunga taasisi za elimu ni ya kutamausha kwa wadau husika, ina manufaa vilevile kwa kuwa inatoa nafasi kwa Wizara ya Elimu kusuluhisha matatizo ambayo kwa muda mrefu, yamelemaza sekta hiyo muhimu.

Ni wakati mwafaka, kwa mfano, kwa Wizara ya Elimu kusuluhisha suala la msongamano na ukosefu wa miundo msingi katika shule za umma.

Ni dhahiri kuwa sera ya elimu bila malipo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ilisaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na kuendelea na masomo. Hata hivyo, sera hiyo pia ilisababisha misongamano katika shule za umma ambazo tayari zilikuwa zinakabiliwa na matatizo ya miundomsingi, hivyo kushusha zaidi viwango vya elimu nchini.

Ripoti kuhusu miundomsingi duni ambayo imesababisha hata maafa ya wanafunzi shuleni zimegonga vichwa vya habari mara kwa mara na hakuna kilichofanywa kufikia sasa kuboresha hali hiyo.

Wanafunzi, hasa kutoka maeneo ya mashinani wamelazimika kustahimili mazingira duni ya elimu, ikiwemo kusomea katika madarasa yaliyofurika maji au hata chini ya miti.

Ni bayana kuwa endapo mradi wa kuwapa vipakatalishi uliopigiwa debe mno ungefanikishwa kikamilifu, ungesaidia pakubwa hasa wakati huu ambapo watoto wamelazimika kukaa nyumbani.

Huku mambo yakibadilika na ulimwengu kukumbatia mfumo wa kielektroniki na kidijitali, huenda ni wakati mwafaka kwa wadau katika sekta ya elimu kufanya mageuzi muhimu yatakayoboresha viwango vya elimu nchini.

Hakuna njia bora zaidi ya kufanikisha hayo ila kwa serikali kupitia Wizara ya Elimu kutumia muda huu ambapo wanafunzi wangali nyumbani, kuboresha vituo vya elimu katika viwango vyote kuanzia chekechea, shule za upili, vyuo vikuu na hata vyuo vya kiufundi.

[email protected]

You can share this post!

Wanaume watahadharishwa kuhusu corona

Ciro Immobile anusia rekodi ya ufungaji barani Ulaya

adminleo