• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:46 PM
CHEPNG’ETICH: Macho yangu ni kwa rekodi ya dunia na mawazo yangu ni kwa dhahabu ya Olimpiki

CHEPNG’ETICH: Macho yangu ni kwa rekodi ya dunia na mawazo yangu ni kwa dhahabu ya Olimpiki

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa dunia katika mbio za kilomita 42, Ruth Chepng’etich anaamini kwamba ana kila kitu kinachohitajika kuvunja rekodi ya dunia katika mbio za marathon katika siku za hivi karibuni.

Mkenya Brigid Kosgei ndiye kwa sasa mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon kwa muda wa saa 2:14:04. Aliuweka muda huo mnamo 2019 katika Chicago Marathon.

Chepng’etich ambaye kwa sasa hujifanyia mazoezi katika eneo la Ngong, anasema kwamba anahitaji tu kumakinika zaidi, kuimarisha kasi yake na kuboresha viwango vyake vya mazoezi ili kumpiga kumbo Kosgei.

Muda wake bora zaidi katika marathon ni saa 2:17:08 aliouweka wakati wa Dubai Marathon mnamo Januari 2019.

“Kuvunja rekodi ya dunia ni jambo ambalo limenijia akilini mara nyingi na kwa sasa nalenga kufanikisha ndoto hiyo katika siku za hivi karibuni. Japo sitatambua mbio nitakazotumia kama jukwaa mwafaka la kufikia malengo hayo, naamini kwamba nitawezeshwa kupanga jinsi ya kutekeleza kila azimio,” akasema Chepng’etich katika mahojiano yake na gazeti moja la humu nchini.

Mbali na kuvunja rekodi ya dunia, Chepng’etich ambaye ni miongoni mwa wanariadha walionufaika na msaada wa vifaa na jezi za kufanyia mazoezi kutoka kwa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (NOC-K), alifichua ukubwa wa maazimio yake ya kunyanyua nishani ya dhahabu katika Olimpiki zijazo jijini Tokyo, Japan.

Chepng’etich, 26, ni sehemu ya wanariadha wa humu nchini walioteuliwa mnamo Januari kuwakilisha Kenya kwenye Olimpiki za Tokyo katika kitengo cha mbio za marathon.

Atatoana jasho na Wakenya wenzake Kosgei na Vivian Cheruiyot ambaye atakuwa akishiriki mbio za marathon kwa mara ya tano tangu astaafu kwenye mbio za mita 10,000.

Sally Chepyego na bingwa wa Frankfurt Marathon, Valary Aiyabei walipangwa na NOC-K kwenye kikosi cha akiba.

“Nashukuru NOC-K kwa vifaa vya mazoezi ambavyo vitanisaidia kuboresha uthabiti wa mikono na miguu yangu. Nasubiri Olimpiki kwa hamu kubwa huku nikiongozwa na imani kwamba nitajizolea medali ya dhahabu na michezo hiyo itanipa jukwaa la kuvunja rekodi ya dunia,” akasema Chepng’etich.

You can share this post!

EPL: Liverpool kuagana rasmi na afisa mkuu mtendaji Peter...

Viongozi wa Pwani walalama kuhusu unyakuzi ardhi ya umma

adminleo