• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 2:13 PM
JAMVI: Kura ya Seneti yakuna bongo za Uhuru, Raila

JAMVI: Kura ya Seneti yakuna bongo za Uhuru, Raila

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya maseneta kukosa kuupitisha Mfumo wa Ugavi wa Mapato kwa Serikali za Kaunti Jumanne, inatishia ndoto na malengo ya baadhi ya vigogo wa kisiasa wanaolenga kuwania urais 2022.

Miongoni mwa vigogo hao ni kiongozi wa ODM Raila Odinga, kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka na Seneta Gideon Moi (Baringo) ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Kanu.

Hatua hiyo pia inaonekana kumweka hatarini kisiasa Rais Uhuru Kenyatta, kuhusu ikiwa baadhi ya maeneo yaliyokosa kuupitisha mfumo huo yatamuunga mkono yule atakayemwidhinisha kuwa mrithi wake.

Kabla ya kura hiyo, Mabw Odinga na Musyoka walikuwa wamewarai maseneta katika vyama vya ODM na Wiper kuupitisha mfumo huo, unaojikita katika idadi ya watu kwenye maamuzi ya kiwango cha fedha ambacho kaunti husika inapaswa kutengewa na Serikali ya Kitaifa.

Kwenye taarifa yake, Bw Odinga alisema kuwa licha ya mageuzi kadhaa kufanyiwa mfumo huo, “nguzo kuu ya ugavi wa raslimali ni idadi ya watu, hivyo akairai Seneti iupitishe.”

Ni kauli ambayo pia ilitolewa na Bw Musyoka, aliyeshikilia kuwa “fedha zinapaswa kugawanywa kwa msingi wa idadi ya watu kwani ndio wanaozitumia.”

Licha ya rai zao, viongozi hao wamejipata matatani, baada ya maseneta kutoka kaunti zilizo katika maeneo yanayowaunga mkono kuwakaidi.

Katika chama cha ODM, baadhi ya maseneta waliomkaidi Bw Odinga ni Cleophas Malala (Kakamega), George Khaniri (Vihiga), Ekal Malachi (Turkana), Sam Ongeri (Kisii), Ledama Ole Kina (Narok), Stewart Madzayo (Kilifi), Issa Juma (Kwale), Mwinyihaji Faki (Mombasa) kati ya wengine.

Ni maseneta kadhaa pekee kutoka chama hicho kama James Orengo (Siaya), Moses Kajwang (Homa Bay), Fred Outa (Kisumu) kati ya wengine ambao walizingatia wito wa Bw Odinga.

Katika chama cha Wiper, maseneta Mutula Kilonzo Junior (Makueni), Enock Wambua (Kitui) na Boniface Kabaka (Machakos) walimkaidi Bw Musyoka.

Bw Moi pia alijipata pabaya, baada ya Seneta Ltumbesi Lelegwe (Samburu) kumkaidi, licha ya Kanu kuwa na mkataba wa ushirikiano wa kisiasa na Chama cha Jubilee (JP).

Rais Kenyatta vilevile alipata pigo kisiasa baada ya maseneta Kindiki Kithure (Tharaka Nithi), Anwar Loitiptip (Lamu), Kipchumba Murkomen, Mahamud Mohamed (Mandera), Wario Juma (Tana River) na Philip Mpaayei (Kajiado) kumkaidi, licha ya kuchaguliwa kwa tiketi ya Jubilee.

Maseneta hao wanaegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao umekuwa ukimpigia debe Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022.

Kutokana na mwelekeo huo, wadadisi wa siasa wanasema kuwa huenda ukaidi huo wa wazi ukaashiria kuwa vigogo hao wako hatarini kiaiasa, hasa wanapopania kuwania urais 2022.

Kwa mujibu wa Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa, matokeo hayo pia yanazua taswira kuwa huenda kukawa na mabadiliko makubwa kwenye miungano ya kisiasa kabla ya uchaguzi huo.

“Matokeo hayo bila shaka yanaonyesha kuna uwezekano mkubwa kwa mipangilio mipya ya kisiasa, ikiwa maseneta wanaweza kuwakaidi viongozi wa vyama vyao kwa njia ya wazi bila kuogopa matokeo ya malengo yao kisiasa,” akasema Bw Muga.

Baadhi ya maseneta wa Jubilee waliopinga mfumo huo, walisema walifanya hivyo ili “kuzilinda jamii ndogondogo na zile za wafugaji dhidi ya kuendelea kudhulumiwa na jamii kubwa.”

Kwenye mahojiano baada ya kikao hicho kilichojaa hisia na majibizano makali, Bw Murkomen alisema msimamo wake ni kuhakikisha jamii hizo zinalindwa dhidi ya kuendelea kudhulumiwa, hasa kwenye mfumo wa ugavi wa raslimali za kitaifa.

“Mjadala huu unaturejesha hadi wakati wa uhuru, ambapo jamii zenye idadi kubwa ya watu ziliungana kuhakikisha jamii ndogo zinatengwa. Hapo ndipo tulipo sasa. Kama walivyofanya watangulizi wetu, tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha tunalinda maslahi ya watu wetu,” akasema Bw Murkomen.

Seneta huyo alikuwa miongoni mwa maseneta ambao waling’olewa kutoka nyadhifa zao za uongozi kwenye Seneti na Jubilee kwa tuhuma za “kumkaidi” Rais Kenyatta.

Wadadisi wanasema kuwa nafasi ya Bw Odinga inahatarishwa na hatua ya kujitokeza kwa baadhi ya viongozi wa Pwani kuwakosoa wenzao wa eneo la Luo Nyanza kwa madai ya “kuwasaliti.”

Bw Odinga amekuwa akipata uungwaji mkono katika eneo hilo kwa muda mrefu na viongozi wengi wamechaguliwa kwa tiketi ya ODM.

Lakini Alhamisi, wabunge kumi wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ kutoka Pwani walitishia kulishinikiza wenzao wahame ODM, wakikitaja chama hicho kuwa “chenye wasaliti.”

Wakiongozwa na mbunge Owen Baya (Kilifi Kaskazini), walisema watavunja ushirikiano wao na ODM na kutafuta washirika wapya kisiasa.

“Tunawaonya maseneta kutoka eneo la Luo Nyanza kwamba mwelekeo wa kisiasa waliochukua huenda ukawa mwanzo wa mwisho wa ushirikiano wetu na ODM,” akasema Bw Baya.

Kulingana na Bw Kiprotich Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa, umefika wakati ambapo vigogo hao wanafaa kutathmini athari za mielekeo hiyo.

“Mwelekeo huo unaashiria kwamba wana mengi ya kufanya kuhakikisha wamedumisha uungwaji mkono kisiasa katika ngome zao, la sivyo huenda wakapoteza wakikimbia kubuni miungano mipya kisiasa,” akasema.

You can share this post!

Jubilee yachafua Katiba

Mwili wa aliyekufa maji akipiga picha wasakwa

adminleo