Hawa ndio matapeli wa Kiswahili waliomkera Abdalla Mwasimba
NA BITUGI MATUNDURA
USIKU wa kuamkia siku ya Jumatano Julai 29, 2020 tasnia ya Kiswahili – hasa taaluma ya utunzi na ughani wa mashairi iliamkia tanzia, kutokana na mauko ya malenga msifika Mzee Abdala Mwasimba.
Mapema Oktoba 2011, nilikutana Mzee Mwasimba katika kongamano la Kiswahili lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA) jijini Nairobi.
Hapo awali, nilikuwa nimepata fursa ya kutagusana na Mzee Mwasimba nilipokuwa mhariri na mfasiri wa habari katika Shirika la Habari la Kenya (KBC) mapema miaka ya 2000.
Vilevile, nilikuwa nimekwisha kutangamana na malenga huyu kwa karibu sana nilipokuwa mwanahabari wa gazeti la Taifa Leo baina ya 2009 – 2010 kabla ya kuiaga taaluma hiyo na kuingia katika akademia.
Kutokana na mazoea yangu ya kuhojihoji – si kwa sababu ya kukera – bali kwa kutaka kujua, nilianza kumdadisi mtunzi huyu kuhusu masuala ya taaluma ya Kiswahili.
Katika mdahalo wetu uliotukumbusha utangamano wetu katika vyombo vya habari, alitoa kauli ya kushangaza mno – ambayo iliniacha na mchanganyiko wa hisia za hamaki na wahka.
Mzee Mwasimba alisema kwamba Kiswahili kimekwisha ‘kutekwa nyara’ na makundi fulani ya watu kiasi kwamba ilikuwa vigumu mno kwa mchango wao (yeye na wazee wengine ambao hawakubahatika kupata elimu ya vyuo vikuu) kutambuliwa.
Na hata pale wanapotambuliwa, utambuzi huo huja shingo upande. Mjadala wetu uliponoga, alipandwa na mihemko ambayo ilitishia kuvuruga mazungumzo yetu.
Aliwaomboleza kwa huzuni kuu watangulizi wake waliokwisha kufariki bila mchango wao kutambuliwa – ama na serikali au asasi nyingine za elimu – licha ya kwamba walichangia sana katika kulisukuma gurudumu la maendeleo ya Kiswahili.
Magunge aliowaomboleza kwa huzuni kuu ni pamoja na Mathias Eugen Mnyampala, Hassan Mwalimu Mbega, Mzee Sheikh Ahmad Nabhany, Athumani Kipanga miongoni mwa wengine. Aliwashutumu baadhi ya wasomi hasa wenye shahada za vyuo vikuu kwa kuwapuuza wazee wanaozifahamu kindakindaki mila na tamaduni za Mswahili.
Alisema kwamba utokeapo mradi – au izukapo midahalo kuhusu masuala mbalimbali, kwa mfano ubunaji wa istilahi, wasomi teule huwaweka pembeni wazee wenye uwezo wa kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Kiswahili.
Watangulizi
Kwa namna moja au nyingine, nilikubaliana na hoja na mikondo ya fikra ya Mzee Mwasimba – hasa alipomtaja marehemu Mzee Ahmad Sheikh Nabhany wa Mombasa aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya leksikoni ya Kiswahili kuwili. Kwanza, kiutendaji, na pili kinadharia.
Mzee Nabhany aliibuka na nadharia yake inayopendekeza kwamba kabla ya kukimbilia kukopa au kutohoa istilahi kutoka lugha za kigeni, ni muhimu kwanza kuchunguza na kupekua lahaja za Kiswahili na lugha nyingine za kiasili.
MzeeNabhany aliibuka na nadharia iliyounga mkono ukuzwaji wa leksikoni ya Kiswahili kama hatua ya awali ya kustawisha leksikoni ya Kiswahili.
Iwapo istilahi hiyo haipo na haiwezi kubuniwa kutokana na lugha zetu za kiasili, basi tunaweza kukopa. Katika kitabu chake – Kandi ya Kiswahili (2012), Mzee Nabhany ameorodhesha maneno ya Kiarabu yaliyoingia katika Kiswahili sanifu ambayo yana visawe vyake katila lugha za kiasili.
Mwasimba pia alisema kuwa Kiswahili kimetekwa nyara na ‘matapeli’. Alisema, kuna matapeli wanaong’ang’ania miradi ya kutafsiri ilhali uwezo, ujuzi na utaalamu wao ni wa kutiliwa shaka.
Inasikitisha sana kwamba Mzee Mwasima amefariki kabla ya kuenziwa akiwa hai. Tulikuwa na mipango ya kumuenzi lakini ikavurugwa na janga la corona. Buriani Mzee Mwasimba.Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka