MATHEKA: Serikali yazidi kuvuruga Katiba, kuleta udikteta
Na BENSON MATHEKA
KAULI ya waziri wa Usalama, Fred Matiang’i kwamba Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki atakuwa akithibitisha maagizo ya mahakama kabla ya kutekelezwa, linadhihirisha kiwango ambacho serikali ya Jubilee imeua na kudharau Idara ya Mahakama, utawala wa sheria na kukumbatia ukiukaji wa haki za wanyonge.
Agizo hilo sio la kikatiba na linathibitisha chuki ya serikali ya Jubilee kwa idara ya mahakama na kujitolea kwa wenye mamlaka kukadamiza haki za masikini na kuepuka adhabu.
Ni agizo linalomfedhehesha Bw Matiang’i, Bw Kihara na serikali wanayohudumia. Hii inajiri baada ya serikali kulaumiwa vikali kwa kuendelea kukiuka maagizo ya mahakama ambayo Mwanasheria Mkuu huwa ameshtakiwa kwa niaba ya serikali.
Kwa upande mwingine ni Wizara ya Usalama inayotumiwa kutekeleza maagizo ya mahakama yawe yametolewa kwa watu binafsi au makundi ya watu dhidi ya serikali au dhidi ya watu au makundi.Bw Kihara amelaumiwa kwa kukataa kuruhusu idara za serikali kukataa kutii maagiza ya mahakama ya kulipa fidia kwa watu wanaodhulumiwa na serikali.
KINAYA
Hivyo basi, ni kinaya kwa Bw Matiang’i kuagiza mshtakiwa kuthibitisha agizo dhidi yake na kuamua linalofaa kutekelezwa ilhali maagizo yote ya Mahakama yanafaa kutekelezwa yakikosa kupingwa kwa kukata rufaa.
Kisheria, ni Msajili Mkuu wa Mahakama anayefaa kuthibitisha maagizo ya mahakama na kwa kuhamishia jukumu hilo hadi ofisi ya Mwanasheria Mkuu, ambaye huwa analinda maslahi ya serikali, ni kutelekeza utawala wa sheria na haki.
Ni juzi tu ambapo serikali iliweka Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) chini ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu katika kilichoonekana wazi kuwa juhudi za kuzima uhuru wa Mahakama.
Uamuzi huo ulijiri baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukataa kuapisha majaji 41 walioteuliwa na tume hiyo. Maamuzi haya yote yanatokana na ushauri wa Mwanasheria Mkuu.
Hivyo basi, kwa kuagiza Mwanasheria Mkuu kuwa akiamua maagizo ya mahakama yanayofaa kutekelezwa, Bw Matiang’i aliashiria kuwa Mahakama iko chini ya ofisi hiyo ambayo imekuwa ikilaumiwa kwa kupotosha serikali.
Japo ni kweli baadhi ya watu wamekuwa wakitumia maagizo feki ya mahakama kuwadhulumu maskini, sio jukumu la Mwanasheria Mkuu kuthibitisha uhalisia wa maagizo hayo kwa sababu huwa hayatolewi na ofisi yake.
KUTETEA DHULUMA
Kilicho dhahiri ni kuwa Bw Matiang’i anataka kutetea serikali kwa dhuluma ilizotendea wakazi wa mitaa kama Kariobangi na Ruai ilipobomoa makazi yao usiku wakati wa mvua kwa kuashiria kwamba maagizo waliyokuwa nayo yalikuwa feki.
Hata hivyo, hatua yake haiwezi ikatakasa dhuluma ambazo serikali imetendea maskini kupitia ushauri wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu, ambaye anatwika au amejitwika jukumu la Mahakama.Hii inaonyesha kwamba kwa serikali ya Jubilee, mahakama huru ni inayokadamiza maskini na kulinda walio mamlakani na matajiri.