Corona yafichua visiki katika sekta ya matatu vina suluhu
Na SAMMY WAWERU
Kwa muda mrefu sekta ya uchukuzi hasa matatu imehusishwa na matukio mengi ya kutoridhisha.
Ni sekta inayosaidia kurahisisha shughuli za usafiri na uchukuzi, ila imesheheni ukiritimba, vituko na sarakasi za kila aina.
Kuanzia matukio ya kunyang’anya abiria chenji baada ya kulipa nauli, wizi wa simu na pia makanga au utingo kutandika watu si mageni hapa nchini.
Matatu, ni sekta inayotajwa kuongoza katika ukiukaji wa sheria za trafiki na kusababisha ajali kiholela.
Isitoshe, maafisa wa trafiki wametambua kwamba ni mtandao wa kufyonza pesa kupitia makosa duni. Idara ya trafiki imetajwa kuwa fisadi zaidi nchini.
Licha ya kuwa kati ya nguzo kuu katika ukuzaji wa uchumi kupitia ushuru na kubuni nafasi za ajira, Wizara ya Uchukuzi na ile ya Usalama wa Ndani zimeonekana kulemewa kudhibiti matatu.
Bw John Michuki (ambaye kwa sasa ni marehemu) na aliyewahi kuhudumu katika Wizara ya Uchukuzi na Usalama wa Ndani, alibuni sheria maalum kuongoza sekta ya matatu, maarufu kama Sheria za Michuki.
Aidha, alishinikiza utekelezaji wa sheria hizo wakati akiwa mamlakani kama Waziri.
Sheria hizo ni pamoja na kuwepo kwa kidhibiti mwendo katika kila matatu, kuwepo kwa mikanda ya usalama, ubebaji wa abiria bila kuzidisha, michirizi ya rangi ya manjano iliyoandikwa gari linakohudumu na idadi ya abiria, vifaa vya huduma za dharura, miongoni mwa nyinginezo.
Kanuni hizo zilitekelezwa japo kwa muda mfupi. Idara husika, zimekuwa zikijaribu juu chini kuzifufua bila mafanikio.
Itakumbukwa kwamba baada ya Dkt Fred Matiang’i kuteuliwa Waziri wa Usalama wa Ndani alijaribu kadri awezavyo kufufua Sheria za Michuki ila jitihada zake hazikuzaa matunda.
“Huu wazimu unaoshuhudiwa katika sekta ya matatu nchini sharti ufikie kikomo,” Dkt Matiang’i alisema wakati akijaribu kufufua sheria hizo.
Kimsingi, ni sekta iliyooza kwa sababu ya utovu wa nidhamu na iliyotekwa nyara na waliowekeza.
Licha ya Sheria za Michuki kugonga mwamba kuafikiwa, tangu Kenya ithibitishe kuwa mwenyeji wa Covi-19 sehemu yazo inatakelezwa bila pingamizi.
Kati ya sheria na mikakati iliyowekwa na Wizara ya Afya kudhibiti janga la corona ni matatu kutakiwa kupunguza idadi ya abiria wanaosafarisha mara moja, hadi asilimia 60.
Hii ina maana kuwa matatu ya jumla ya abiria 14 sasa inabeba abiria 8, amri hii ikitakiwa kutekelezwa katika magari mengine ya umma.
Chini ya uongozi wa Mutahi Kagwe, Waziri wa Afya, kwa ushirikiano na Waziri wa Uchukuzi James Macharia na Dkt Fred Matiang’i wa Usalama wa Ndani, imekuwa lazima kama ibada matatu kupunguza idadi ya abiria.
Hata ingawa wananchi wanafukua mfuko zaidi kugharamia safari kufuatia ongezeko la nauli lilosababishwa na hitaji hilo la idara ya afya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, ni ishara kuwa sekta ya matatu na uchukuzi kwa jumla inaweza kudhibitika.
Sheria zipo, zile za trafiki, ila utani na waliowekeza katika sekta hiyo pamoja na wadau husika wamezishika mateka.
Janga la Covid-19 limedhihirisha wazi sheria ni msumeno na hukata kwa ncha zote, bila kubagua maskini wala tajiri.
Awali, matatu zilipakia abiria kupita kiasi jambo lililochangia kutokea kwa mikasa ya ajali na iliyosababisha maafa na majeraha.
Huku kila mmoja akipiga Dua kwa Mwenyezi kutuondolea gonjwa la corona, unapoingia kwenye matatu ina mpangilio kabambe, ambapo hakuna mhudumu anayezidisha kiwango cha abiria.
Hongera kwa idara ya afya kusimama kidete na ngangari na sheria na mikakati kuzuia msambao wa corona, imedhihirika Wakenya kwa jumla tukishirikiana utepetevu na utovu wa nidhamu katika sekta ya matatu utafikia kikomo.
Hakuna anayehitaji kukumbushwa matatu imejaa, na isitoshe wahudumu haohao ndio wanakutahadharisha. Ni wahudumu wachache tu waliotia maskio yao nta, wenye tamaa na ubinafsi wanapokiuka sheria zilizowekwa na Wizara ya Afya kwa ushirikiano na ile ya Uchukuzi, ya Usalama wajibu wake ukiwa ni kuwakamata na kuwachukulia hatua kisheria.
Ili kutia muhuri mikakati kudhibiti msambao wa Covid-19 katika matatu, wahudumu wametakiwa kuondoa viti vinavyosalia wazi.
Aidha, ni pendekezo ambalo hawajalipokea vyema. “Tangu corona iingie nchini, sheria za kudhibiti matatu zikatolewa tunaendelea kukadiria hasara. Kutuamuru tuondoe viti vilivyo wazi ni sawa na kuweka chumvi kwenye kidonda kinachouguza,” mmoja wa mameneja wa mabasi yanayohudumu kati ya mtaa wa Githurai na jiji la Nairobi akaambia Taifa Leo Dijitali.
Kando na matatu, tuktuk, teksi na hata bodaboda pia zimepunguza idadi ya abiria wanaobebwa mara moja.
Waziri wa Uchukuzi Bw James Macharia amesisitiza kwamba serikali haitalegeza kamba sheria zilizowekewa wahudumu wa matatu kuzuia kuenea corona. “Tunahimiza maafisa wa usalama kuwachukulia hatua wahudumu wanaokiuka sheria na mikakati tuliyopendekeza,” Waziri akasema.
Alisema hayo Alhamisi wakati akitoa mpangilio wa safari za ndege kuruhusiwa kuingia ndani na kutoka nje ya nchi. Kuhusu mikakati ya matatu, alisema serikali imeshirikisha wadau husika wote.
Amri ya kupunguza abiria ikielekezwa katika kuhakikisha kila gari la umma limewekwa kidhibiti mwendo, na mikanda ya usalama, kimsingi sheria za trafiki zitaheshimika na kupunguza mikasa ya ajali barabarani inayochangiwa na matatu.