• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Chelsea yalia Septemba 12 ni mapema mno EPL kuanza

Chelsea yalia Septemba 12 ni mapema mno EPL kuanza

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Frank Lampard amewakosoa waratibu wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kudai kwamba Septemba 12, 2020 itakuwa mapema sana kwa kikosi chake cha Chelsea kuanza kunogesha soka ya msimu ujao wa 2020-21 hasa ikizingatiwa ugumu wa ratiba uliopo mbele yao.

Siku ya kuanza kwa msimu mpya wa EPL ilithibitishwa na vinara wa soka ya Uingereza (EFL) mwezi uliopita.

Ingawa hivyo, Lampard anahisi kwamba vijana wake hawatakuwa na muda wa kujiandaa vya kutosha kwa muhula ujao iwapo watapiga hatua zaidi kwenye kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Chelsea watakuwa wageni wa Bayern Munich katika mechi ya mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora katika UEFA wikendi hii uwanjani Allianz Arena. Mshindi atakutana na ama na Barcelona au Napoli katika hatua ya robo-fainali.

Hata iwapo watabanduliwa kwa kushindwa kubatilisha kichapo cha 3-0 walichopokezwa na Bayern katika mkondo wa kwanza, Chelsea watakuwa na siku 35 pekee za kupumzika kabla ya kurejea kwa kampeni za msimu mpya wa EPL.

“Wachezaji wanahitaji muda wa kupumzika vya kutosha ndipo waweze kushindana vilivyo katika mojawapo ya ligi ambapo viwango vya ushindani ni vya juu zaidi. Vinginevyo, tutakuwa tukiwaweka katika hatari ya kupata majeraha mabaya zaidi,” akasema Lampard.

Inaripotiwa kwamba vikosi vya EPL vilipoafikiana kuhusu tarehe ya kuanza kwa msimu mpya, iliwekwa wazi kwamba likizo ya hadi 30 ingetolewa kwa Chelsea na timu nyinginezo ambazo zingesalia katika kampeni za mwisho wa msimu huu kwenye soka ya bara Ulaya.

Manchester City pia wangali katika kivumbi cha UEFA ambacho kitatamatika rasmi mnamo Agosti 23. Kwa upande wao, Manchester United na Wolves bado wanashiriki kipute cha Europa League kitakachokunja jamvi mnamo Agosti 21.

Siku moja kabla ya kuwaongoza Chelsea kuvaana na Arsenal katika fainali ya Kombe la FA mnamo Agosti 1 uwanjani Wembley, Chelsea walipatwa na pigo la kuumia kwa Willian na Ruben Loftus-Cheek mazoezini. Kikosi hicho kilijipata pia katika ulazima wa kukosa kujivunia kikamilifu huduma za beki Cesar Azpilicueta na Christian Pulisic waliopata majeraha wakati wa mechi dhidi ya Arsenal.

“Nitajisadikisha kwamba vinara wa EPL watazingatia hali yetu kwa sasa na kutoa ratiba nafuu zaidi itakayotuwezesha kuanza kampeni za msimu ujao kwa kiwango sawa na wengine. Hata kama tutabanduliwa na Bayern kwenye UEFA, bado nahisi kwamba Septemba 12 ni mapema sana kwa Chelsea kujitosa tena ulingoni,” akasema Lampard.

Kwa upande wake, kocha Pep Guardiola wa Man-City amesema wana kiu ya kutwaa taji la UEFA msimu huu baada ya kuridhika na mafanikio ya kufuzu kipute hicho muhula ujao.

Man-City kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Real Madrid katika marudiano ya hatua ya 16-bora mnamo Ijumaa ugani Etihad huku wakijivunia ushindi wa 2-1 kutokana na mechi ya mkondo wa kwanza.

Ushindi au sare dhidi ya Real katika gozi hilo itawapa Man-City tiketi ya robo-fainali dhidi ya mshindi kati ya Olympique Lyon na Juventus.

Man-City hawajawahi kusonga mbele zaidi ya hatua ya nusu-fainali kwenye kivumbi cha UEFA ambacho kocha Guardiola alikinyanyua mwisho akidhibiti mikoba ya Barcelona mnamo 2011.

Mapambano yote ya robo-fainali, nusu-fainali na fainali ya UEFA yatachezewa jijini Lisbon, Ureno kati ya Agosti 12-23. Mechi za robo-fainali zitaanza kupigwa Agosti 12 katika uwanja wa Jose Alvalade. Nusu-fainali zitaandaliwa kati ya Agosti 18-19 uwanjani Sport Lisboa Benfica kabla ya uga huo kuwa mwenyeji wa fainali mnamo Agosti 23.

Chelsea na Man-City watakutana katika nusu-fainali iwapo watafaulu kuwabwaga wapinzani wao kwenye hatua ya 16-bora na robo-fainali.

Bayern na Man-City ambao wanawania ufalme wa UEFA kwa mara ya kwanza katika historia, ndio wanaopigiwa upatu wa kutia kapuni taji la kipute hicho msimu huu.

“Sioni kikubwa kitakachotuzuia kunyanyua ubingwa wa UEFA msimu huu iwapo tutawaangusha Real,” akasema Guardiola kwa kukiri kwamba atakuwa amefeli pakubwa iwapo atabanduka uwanjani Etihad bila ya kunyanyua taji la UEFA.

Atletico Madrid waliowabandua Liverpool, watakutana na RB Leipzig ya Ujerumani kwenye robo-fainali huku Atalanta ya Italia ikivaana na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa.

You can share this post!

Corona imetufilisiha, yasema Barca

Drogba kuwania urais wa soka Ivory Coast

adminleo