Mombasa hakuna raha tena – utafiti
Na WANDERI KAMAU
KAUNTI ya Mombasa ambayo ni maarufu kwa kaulimbiu yake ya ‘Mombasa Raha’ imeibuka miongoni mwa kaunti tano nchini ambapo wakazi wameripotiwa kutokuwa na raha.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la Infotrak, Kaunti ya Makueni ndiyo iliibuka eneo lenye wakazi wenye raha zaidi.
Utafiti ulizingatia hali ya mandhari ya kisiasa na jinsi wakazi wanavyohusishwa katika mipango ya maendeleo.
Kaunti nyingine ambazo zilibainika kuwa na idadi kubwa ya watu wasio na furaha ni Taita Taveta, Nairobi, Trans Nzoia na Siaya.
Ilibainika kiwango cha furaha ya wakazi wa Kaunti ya Mombasa ni asilimia 52.6 pekee, na kuweka kaunti hiyo katika nafasi ya 44 kati ya kaunti 47.
Wakazi wa Taita Taveta walikuwa na kiwango cha furaha cha asilimia 48.9 pekee, hali iliyowafanya kuibuka kuwa wenye huzuni zaidi miongoni mwa kaunti zote.
Kaunti tatu za eneo la Nyanza, ambazo ni Homa Bay, Nyamira na Siaya pia zilitajwa kuwa miongoni mwa kaunti kumi zenye kiwango kikubwa cha watu ambao hawana furaha.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Infotrak, Bi Angela Ambitho, alisema utafiti huo ulizingatia mandhari ya kisiasa katika kaunti na jinsi wakazi wanavyohusishwa katika mipango ya maendeleo.
“Hizi ni kaunti ambazo zinajitahidi sana kutekeleza miradi kama ya barabara lakini hazijahusisha wakazi wao jinsi Makueni ilivyofanya. Kwa hivyo imebainika haya mambo yanayochukuliwa kuwa madogo huwa yanaathiri hisia za wakazi,” akaeleza.
Hii inaashiria kuwa, mafanikio ya mfumo wa ugatuzi unaonekana kuchangia pakubwa hali ya furaha miongoni mwa Wakenya wengi.
Hata hivyo, utafiti huo umefanywa wakati ambapo janga la corona linatatiza sana wakazi wa mijini.
Utafiti uliitaja Kaunti ya Makueni kuwa yenye kiwango cha juu cha furaha miongoni mwa wenyeji wake.
Kaunti zilizofuata ni Pokot Magharibi, Machakos, Bomet, Kwale, Elgeyo Marakwet, Marsabit, Uasin Gishu na Kericho. Gavana Kivutha Kibwana wa Makueni amekuwa akisifiwa katika majukwaa mengi kutokana na utendakazi wake bora, hasa uimarishaji wa sekta ya afya.