MATHEKA: Ukatili kuchelewesha malipo ya Kazi Mtaani
Na BENSON MATHEKA
ALIPOZINDUA mpango wa kazi mitaani, Rais Uhuru Kenyatta alisema kwamba lengo lake lilikuwa ni kulinda maelfu ya vijana walioathiriwa kiuchumi na janga la corona.
Mpango huo ulifanyiwa majaribio katika miji ya Nairobi na Mombasa ambako vijana walisajiliwa kusafisha mitaa kama njia moja ya kuhakikisha usafi wa mazingira.
Chini ya mpango huo, serikali inalenga vijana katika mitaa ya mabanda ambao wameathiriwa sana kiuchumi na janga la corona.
Baada ya majaribio, serikali ilitangaza kuwa ungepanuliwa na kufaidi vijana 250,000 katika maeneo ya miji kote nchini. Rais Uhuru Kenyatta alisema kwamba serikali ilikuwa imetenga Sh10 bilioni kufanikisha mradi huu kwa kipindi cha miezi sita hadi Disemba mwaka huu. Wakati wa majaribio ya mradi wenyewe, changamoto ilizuka kuhusu malipo. Mamia ya vijana waliotumiwa katika awamu ya hiyo walilamika kwamba hawakulipwa katika muda ambao walikuwa wameahidiwa.
Waliandamana jijini Nairobi, Kisumu na Mombasa kuonyesha kufadhaika kwao kwa kukosa kulipwa. Maafisa wa serikali walisema kulikuwa na dosari zilizotambuliwa na vijana hao walilipwa ziliporekebishwa.
Hii ilikuwa ni baada ya vijana hao kuandamana, wakidai haki yao. Hata hivyo tatizo hili halikukomea hapo. Waliosajiliwa chini ya mpango huo ambao ni mradi wa serikali ya kitaifa wamekuwa wakilalamika kwamba wanacheleweshewa malipo.
Mtindo umekuwa kwamba ni lazima walalamike ndipo walipwe. Hii inaonyesha kuwa huenda kuna maafisa wa serikali wanaochelewesha malipo hayo makusudi ili kuzitumia pesa hizo kujinufaisha kwanza.
Sio mara ya kwanza pesa zinazotengewa miradi ya serikali kuelekezwa kwa masuala mengine baadhi yakiwa ya maafisa binafsi wa serikali.
Ikizingatiwa hali ngumu ya maisha ambayo vijana hawa wanapitia wakati huu ambao kazi zimeandimika kutokana na janga la corona, inaweza kuwa ukatili wa hali ya juu kuwacheleweshea makusudi malipo yao.
Wengi wao huwa wanafanya kazi hiyo bila hata kutia chochote tumboni na bila vifaa vya kazi. Baadhi huwa wanategemea pesa hizo kulipa madeni waliyo nayo kwa mama mboga na hata kulips kodi ya nyumba na ni makosa kwa afisa wa serikali jijini Nairobi aliyeshiba na kusaza kukataa kuwalipa kwa wakati. Mfumo unaotumiwa kuwasajili vijana katika mpango huo ni mmoja kote nchini na haieleweki ni kwa nini malipo yanaonekana kutolewa kwa ubaguzi. Hii ni kwa sababu sio wote wanaokosa kulipwa kwa wakati.
Kwa vile serikali ilitoa pesa zilizotengewa mpango huu na ilisema dosari zilizogunduliwa katika awamu ya majaribio zilirekebishwa, maafisa wanaohusika wana maswali ya kujibu kwa kuwa sababu wanazotoa haziridhishi.
Katika serikali iliyokolewa na ufisadi na ambayo siasa huingizwa katika kila mradi, ipo haja ya idara inayohusika na mpango huu kupigwa darubini.
Miradi inayolenga kunufaisha vijana imekuwa ikitumiwa kufyoza pesa za umma na sio ajabu huu ukageuzwa kunufaisha wachache wenye ushawishi.
Wakenya hawasahau mpango wa kazi kwa vijana uliokuwa chini ya Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS) ambao ulibadilika kuwa jinamizi mabilioni ya pesa zilipoporwa na kwa hivyo malipo yanapochelewa chini ya mpango wa kazi mitaani, vijana wana sababu ya kuwa na hofu.