• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
ODONGO: Magavana wasizuie wapinzani wao kuanzisha miradi

ODONGO: Magavana wasizuie wapinzani wao kuanzisha miradi

Na CECIL ODONGO

IMEKUWA ni vuta nikuvute kati ya maafisa wa serikali wanaozindua miradi mbalimbali na baadhi ya magavana kuhusu siasa za 2022.

Baadhi ya wakuu wa kaunti wanatilia shaka ziara za kimaendeleo za mawaziri au makatibu wao, wakifasiri safari hizo kuwa za kisiasa zenye lengo la kudidimiza umaarufu wao kabla ya uchaguzi huo.

Huku magavana wakihusika na kuimarisha utoaji wa huduma kwa raia, viongozi wa serikali nao wamekuwa wakihusika na kutathmini au kuhakikisha miradi ya serikali kuu iliyoanzishwa inatekelezwa vilivyo.

Vuta ni kuvute kama hiyo imeshuhudiwa katika Kaunti ya Murang’a kati ya Katibu wa Wizara ya Maji, Joseph Irungu na Gavana wa Murang’a, Mwangi wa Iria.

Bw Irungu amekuwa akizindua uchimbaji wa visima na miradi mingine ya maji huku Bw Iria akionekana kupinga miradi hiyo na kupigania huimarishaji wa kampuni za maji za kaunti kama njia pekee ya kusuluhisha tatizo la maji kwa wakazi.

Gavana huyo aliwahi kunukuliwa akisema Katibu huyo anatumia miradi ya maji kunadi mpango wake wa kuwania ugavana 2022.

Waziri wa Maji, Sicily Kariuki na Gavana wa Nyandarua Dkt Francis Kimemia, pia wamekuwa wakizozana kuhusu miradi ya serikali kuu.

Tofauti na Bw Iria anayemaliza hatamu yake, Dkt Kimemia ameingiwa na wasiwasi kwamba miradi ya serikali kuu inayosimamiwa na Bi Kariuki katika kaunti hiyo huenda ikafifisha umaarufu wake.

Kuna minong’ono kwamba Bi Kariuki analenga kuwania kiti cha ugavana wa Nyandarua japo hajatangaza hilo hadharani.

Mrengo unaongozwa na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na Gavana Wycliffe Oparanya nao umekuwa ukikashifiwa na Kinara wa ANC Musalia Mudavadi, na Seneta wa Bungoma, Moses Wetang’ula kwa kutumia miradi ya kisiasa kujiimarisha kisiasa katika eneo la Magharibi.

Bw Wamalwa na Oparanya wamekuwa wakizindua miradi kama ujenzi wa uwanja wa ndege mjini Kakamega na ufufuaji wa viwanda vya sukari miongoni mwa mingine.

Mabw Mudavadi na Wetang’ula nao wamekuwa wakishutumu serikali kwa kuwatumia wapinzani wao kuwahujumu kisiasa na kuchochea misukosuko katika vyama vyao vya ANC na Ford Kenya.

Katika Kaunti ya Nairobi, Gavana Mike Sonko na msimamizi wa huduma za jiji Mohammed Badi hawapatani kisiasa, Gavana akimlaumu mwanajeshi huyo kwa kuingilia majukumu yake.

Licha ya kutia saini mkataba wa kuhamisha baadhi ya majukumu yake hadi serikali kuu, Bw Sonko anadai alichezewa shere na kuna njama ya kuhakikisha hatekelezi wajibu wake vilivyo muda uliosalia kabla uchaguzi wa 2022.

Hata hivyo, uhasama kati ya mirengo hii miwili haifai kwa sababu cha muhimu ni huduma za maendeleo zimfikie mwananchi wa kawaida.

Ingawa hivyo magavana wanafaa waendesha majukumu yao bila hofu ya kupoteza umaarufu wao mahasimu wao serikalini wanapozindua miradi ya maendeleo maeneo yao.

Kwa upande mwingine mawaziri au makatibu wanafaa wawe waaminifu na kutekeleza miradi ya serikali kuu bila kuitumia kwa malengo yao ya kisiasa.

You can share this post!

MATHEKA: Ukatili kuchelewesha malipo ya Kazi Mtaani

DIMBA: Kinda Jesus hana kifani, aenda mbali

adminleo