Makala

Jinsi wakazi wa mtaa wa mabanda wa Bangladesh wanavyodumisha usafi kuzuia kuenea kwa Covid-19

August 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WINNIE ATIENO

MNAMO Machi, tangu kisa cha kwanza virusi vya corona kuripotiwa kaunti ya Mombasa, zaidi ya wakazi 20,000 kutoka mtaa wa mabanda wa Bangladesh walijikusuru na kuanza kudumisha usafi ili kujikinga dhidi ya ugonjwa hatari wa Covid-19.

Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwekwa kwa sehemu za kuosha mikono pamoja na ufadhili wa bure wa maji na sabuni.

Wakazi na wageni wanaozuru mtaa huo nao hupewa barakoa na sanitaiza ili kujikinga dhidi ya virusi hivyo.

Miezi mitano baadaye, juhudi zao zimezaa matunda baada ya mtaa huo kupigana na virusi hivyo hatari.

Bangladesh imeorodheshwa kama mtaa wa mabanda katika jiji hilo la kitalii ambalo halijakumbwa na kisa chochote cha virusi hivyo.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema visa vya corona katika kaunti ya Mombasa vimeanza kushuka hata hivyo wilaya ya Mvita ingali hatari kwa maambukizi.

Katika mtaa huo wa mabanda, wafadhili wamejizatiti kuhakikisha wakazi wanasalia na maji ili wanawie mikono mara kwa mara.

Katika barabara ya kuingia mtaa huo, soko na sehemu za umma ni baadhi ya maeneo ambayo vifaa vya kuoshea mikono imewekwa huku wakazi na wageni wakilazimishwa kutimiza jukumu hilo.

Wanafunzi wa shule za upili na msingi wajadiliana maswala kuhusu corona kwenye maktaba ya Shofco mtaani Bangladesh. Wanafunzi hao hukutana maktabani kusoma wakati shule zimesalia kufungwa kufuatia janga la corona. Picha/ Winnie Atieno

Vijana wamekita kambi kwenye sehemu hizo ili kuhakikisha agizo la serikali la kuwataka wakazi kuosha mkono linatimizwa.

“Tumeweza kupambana na janga hili kupitia kuosha mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa na kuendeleza kuhubiri dhidi ya kuepuka virusi hivi. Kila mgeni anayeingia mtaa huu tunamlazimu aoshe mikono, tunawapa maji ya bure, sabuni, sanitiza na barakoa kwa hivyo hakuna sababu ya kulegeza kamba,” alisema Bw Joseph Oluoch, afisa mkuu wa kundi la jamii la Shining Hope (Shofco) tawi la Pwani.

Shofco pia inawaletea wakazi hao maji ya matumizi kwa majumba yao ili wasiteseke kusaka bidhaa hiyo adimu kaunti ya Mombasa.

Bw Oluoch alisema ufadhili huo wa maji umewasaidia wakazi kutotembea sehemu mbali wakisaka bidhaa hiyo.

Shofco imekuwa ikiwapa vijana, watu wanaoishi na ulemavu, na kina mama jinsi ya kutengeneza sabuni, sanitaiza na barakoa ambazo zinasambazwa kwa wakazi.

Vijana, watu wanaoishi na ulemavu na kina mama mtaani Bangladesh watengeneza sanitaiza ambazo zitasambazwa kwa wakazi. Hii imekuwa ajira kwao. Picha/ Winnie Atieno

Afisa mkuu wa afya ya umma kaunti hiyo, Bi Aisha Abubakar alisema kijiji hicho kimefaulu kupambana na virusi hivyo kutokana na taratibu kali zilizowekwa na makunzi ya kijamii.

Alisema wakazi wanafuata kanuni za wizara ya afya dhidi ya namna ya kupambana na virusi hivyo jambo lililowasaidia kuepuka visa hivyo.

“Kwa jumla hatujarekodi au kupata visa vingi vya corona katika mitaa ya mabanda isipokuwa Muoroto iambapo kulikuwa na visa viwili. Lakini kama kaunti tumeshirikiana na makundi ya kijamii kuwapa mafunzo ya usafi na imezaa matunda,” alisema Bi Abubakar.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bi Abubakar anasema kampeni walizofanya zimefua dafu ndiposa mitaa ya mabanda haijanakili kisa chochote cha kipindupindu wakati huu wa mvua Mombas

“Bangladesh ndio mtaa mkubwa wa mabanda Kaunti ya Mombasa, lakini wakazi wamejipanga kuhakikisha wanaepuka maambukizi ya virusi vya corona,” aliongeza Bi Abubakar.

Gavana Hassan Joho naye aliwasihi wakazi kuendelea kufuata kanuni hizo ili kuepuka maambukizi.

“Covid-19 iko; msidanganywe kwamba hakuna. Nataka kuwakumbusha umuhimu wa kufuata kanuni za afya ili tupigane na janga hilo. Lazima tukomeshe corona hapa Mombasa,” alisisitiza Bw Joho hivi majuzi.

Mkazi wa Bangladesh Bi Racheal Kanini alisema udumishwaji wa kanuni za afya hususan kuosha mikono miongoni mwa watoto imesaidia kukabiliana na magonjwa mengi hususan kuharisha.

“Watoto wetu wametambua umuhimu wa kuosha mikono, wamekuwa vielelezo bora miongoni mwa jamii. Hatutaki corona hapa ndio maana tunafuata kanuni zote bila pingamizi, ugonjwa huo ni hatari sana. Watu waige mfano wetu,” alisema Bi Kanini.