Yafichuka Ikulu ilihusika kusukuma Elachi ajiuzulu cheo Nairobi
Na COLLINS OMULO
RAIS Uhuru Kenyatta alihusika katika uamuzi wa Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Bi Beatrice Elachi kujiuzulu, kama sehemu ya juhudi za Serikali Kuu kutaka kudhibiti kaunti hiyo, imefichuka.
Duru ziliambia Taifa Leo kwamba mpango wa kumshawishi Bi Elachi aondoke mamlakani ulikuwa unaendelezwa kwa wiki kadhaa Ikuluni chini ya uongozi wa Rais Kenyatta.
Inaaminika kuwa, uamuzi huo ni sehemu ya mipango mingi ya Rais kutaka kudhibiti shughuli za jiji hilo kuu bila usumbufu kutoka kwa upande wowote miezi michache baada ya kumshawishi Gavana Mike Sonko kusalimisha baadhi ya majukumu kwa Serikali Kuu.
Mkutano wa kwanza ulifanyika katika Ikulu mnamo Julai 31, 2020, ambapo iliamuliwa Bi Elachi ajiuzulu wakati ambapo angeambiwa afanye hivyo.
Madiwani wanaofahamu kuhusu mkutano huo wa siri, waliogopa kuuzungumzia wakisema walionywa vikali kutotoboa siri.
Hata hivyo, walisema kuna karata zinazochezwa na hivi karibuni, jambo kubwa litatendeka katika kaunti hiyo.
“Kulikuwa na mkutano ulioitishwa na Rais katika Ikulu na yale ambayo yametokea ni matokeo ya mkutano huo. Lakini maelezo zaidi yatafafanuliwa wakati mipango yote itakapokamilishwa. Kwa sasa jueni tu kwamba hakujiuzulu kwa hiari, aliagizwa kufanya hivyo,” akasema mmoja wa viongozi.
Viongozi ambao walizungumza na Taifa Leo walifichua kuwa, mkutano huo wa kwanza ulioitishwa na Rais Kenyatta ulihudhuriwa pia na Bw Sonko pamoja na madiwani wasiopungua 41 wa Chama cha Jubilee wakiwemo wanaoegemea upande wa Kiongozi wa Wengi, Bw Abdi Guyo.
Bi Elachi hakuhudhuria mkutano huo, sawa na madiwani wachache wanaoegemea upande wake.
“Rais alituambia alitaka kujua kuhusu chanzo cha ghasia ambazo hutokea katika bunge la kaunti na watu wakamweleza wazi wazi. Mkutano ulikuwa wa siri sana na tukaagizwa kutofichua chochote kuuhusu. Aliahidi kutatua tatizo lililopo kabla wiki mbili zikamilike,” duru zikasema.
Imebainika Rais hakuficha msimamo wake kwamba ananuia kurekebisha Nairobi, akamwonya Bw Sonko kwamba pia yeye ataondolewa kama ataendelea kukataa kushirikiana na Bw Badi.
“Alimwambia kwamba alikuwa amezungumza nao wawili mara tatu na kama hatatii, basi hatima yake itakuwa sawa na ya spika,” Taifa Leo ikaelezwa.
Kwa siku kadhaa sasa, Rais Kenyatta amekuwa akizunguka katika sehemu tofauti za Nairobi kukagua miradi inayoendelezwa na NMS.
Matukio haya yamewaacha wadadisi wakijiuliza maswali chungu nzima, ikiwemo kama kuna mpango wa kuvunja serikali nzima ya kaunti hiyo ili shughuli zote zisimamiwe na Idara ya Utoaji Huduma Nairobi (NMS) inayosimamiwa na Jenerali Mohamed Badi.
Jumanne mapema asubuhi, Bi Elachi alitangaza kuwa ameamua kujiuzulu na kumtwika naibu wake, Bw John Kamangu mamlaka kwa muda hadi wakati spika mpya atakapochaguliwa.
“Kwa siku chache zilizopita, tumeshuhudia mizozo mingi na hata matukio ya kutishiwa maisha. Nisingependa kuwa mhusika katika athari yoyote inayoweza kutokea kwa maisha ya mtu hapa,” akaeleza.
Jumanne, Bw Sonko aliendeleza mashambulizi yake dhidi ya Bw Badi kuhusu usimamizi wa kaunti.
Huku akijigamba kwamba yeye ndiye gavana wa jiji kuu, gavana huyo anayekumbwa na kesi ya ufisadi alimkosoa kiongozi wa NMS kuhusu usimamizi wake wa kaunti.