Makala

ONYANGO: Vijana wapewe mitaji ya biashara si Kazi Mtaani

August 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

FEDHA zilizotolewa na Benki ya Dunia kuendeleza mradi wa Kazi Mtaani zinafaa kutumiwa kutoa mikopo kwa vijana ili waanzishe biashara.

Benki ya Dunia Jumatatu ilitangaza kuwa imetoa kitita cha Sh16.2 bilioni zitakazotumiwa kuboresha miundomsingi katika vitongoji duni kupitia mradi wa Kazi Mtaani kote nchini.

Mradi huo ulianzishwa na serikali kama njia mojawapo ya kuwawezesha vijana kujikimu kimaisha wakati huu wa janga la virusi vya Corona ambalo limesababisha maelfu kupoteza ajira na biashara zao.

Kupitia mradi huo, vijana wanaajiriwa kufanya kazi ya usafi katika mitaa mbalimbali.

Kwa mujibu wa ripoti za serikali, mradi huo umesaidia pakubwa kung’arisha vitongoji duni ambavyo vimekuwa vikizongwa na uchafu kwa miaka mingi.

Mradi huo ulianza chini ya miezi mitatu iliyopita na kufikia sasa, umekumbwa na changamoto si haba.

Vijana wamekuwa wakiandamana wakilalamikia kucheleweshwa kwa malipo yao. Serikali haijakuwa ikiwalipa vijana hao ujira wao kwa wakati ufaao.

Malipo ya vijana walionufaika na mradi huo pia yamepunguzwa kutoka Sh653 zilizokuwa zimetangazwa awali na Rais Uhuru Kenyatta hadi Sh450.

Baraza la Kitaifa la Vijana (NYC) wiki iliyopita lililama kuwa, vijana walioshiriki Kazi Mtaani walilipwa Sh2,275 badala ya Sh4,950. Hiyo inamaanisha kuwa walilipwa Sh 206 badala ya Sh450. Malipo ya vijana hao yamekuwa yakipunguzwa kiholela na serikali bila kuwafahamisha vijana wanaoshiriki mradi huo.

Mradi huo pia umekumbwa na sakata ya kuwepo kwa upendeleo ambapo machifu na maafisa wengine wa serikali wamekuwa wakishutumiwa kuajiri marafiki na jamaa zao. Mradi huo umekumbwa na madai ya kuwepo kwa ubaguzi wa kikabila.

Mpango wa Kazi Mtaani unafaa ila hauna manufaa kwa vijana. Vijana hufanya kazi kwa siku 11 kwa mwezi. Hiyo inamaanisha kwamba, kwa mwezi vijana hao wanapokea chini ya Sh6,000.

Kiasi hicho cha fedha hakitoshi kulipa ada ya nyumba, kununua chakula na kusaza hela za mtaji wa biashara.

Vile vile, fedha zinazotumika kulipa vijana hao hazina manufaa yoyote kwa uchumi wa nchi hii.

Je, mradi huo ukiisha vijana hao watajisaidia vipi?

Ukweli ni kwamba, wengi wa vijana wanaoshiriki katika mradi wa Kazi Mtaani walipoteza kazi zao kufuatia janga la virusi vya corona.

Ikiwa serikali inahitaji kuboresha maisha ya vijana hao, basi haina budi kutumia fedha hizo kuwapa mikopo ya kuanzisha biashara zitakazowasaidia kwa muda mrefu.

[email protected]