Michezo

Robert Lewandowski anusia rekodi ya Ronaldo ya kufunga mabao kwenye Uefa

August 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

NYOTA Robert Lewandowski kwa sasa anajivunia kufungia Bayern Munich ya Ujerumani jumla ya mabao 53 kutokana na mechi 44 za mapambano yote ya hadi kufikia sasa msimu huu.

Alifunga bao katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Chelsea katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti 8, 2020 na kuwapa waajiri wake tiketi ya kuvaana na Barcelona katika robo-fainali za kivumbi hicho mnamo Ijumaa ya Agosti 14 jijini Lisbon, Ureno.

Lewandowski, 31, kwa sasa amefunga mabao 13 kutokana na mechi saba za UEFA msimu huu na anasalia na magoli manne pekee kuifikia rekodi ya Cristiano Ronaldo aliyewahi kutikisa nyavu za wapinzani wao wa UEFA mara 17 akivalia jezi za Real Madrid mnamo 2013-14.

Iwapo Bayern watatinga fainali ya UEFA msimu huu, ina maana kwamba Lewandowski ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Poland, atakuwa na mechi tatu zaidi za kuivunja rekodi ya Ronaldo ambaye alishuhudia waajiri wake Juventus wakibanduliwa na Olympique Lyon ya Ufaransa kwenye hatua ya 16-bora mnamo Ijumaa iliyopita.

“Sina lengo la kuvunja rekodi ya Ronaldo. Tuna mechi chache muhimu zilizosalia na nia yangu ni kuendelea kuchangia mabao na kufunga nipatapo fursa. Iwapo nitaifikia rekodi ya Ronaldo katika harakati hizo, ieleweke kwamba hayakuwa maazimio yangu ya tangu mwanzo,” akasema Lewandowski.

Ronaldo ambaye ni mzawa wa Ureno, ndiye mfungaji bora wa muda wote katika soka ya UEFA, akijivunia mabao 130.

Lionel Messi wa Barcelona anamfuata kwa mabao 115 huku Lewandowski akishikilia nafasi ya nne kwa magoli 66, moja mbele ya Karim Benzema wa Real.

Aliyekuwa mvamizi matata wa Real, Raul Gonzalez, 43, anashikilia nafasi ya tatu kwa mabao 71.

Ili kumfikia Ronaldo, ina maana kwamba Lewandowski atalazimika kufunga jumla ya mabao 16 kila msimu katika kipindi cha miaka minne ijayo huku uchukulio ukiwa kwamba Ronaldo hatawahi kupachika wavuni goli lolote tena katika UEFA.

Msimu huu pekee, Leandowski amempiku Ronaldo katika ufungaji wa mabao baada ya kutikisa nyavu za wapinzani mara 53 huku Ronaldo akifunga mabao 36 pekee katika mashindano yote ambayo amewawajibikia Juventus.

Rekodi nzuri ya ufungaji wa Lewandowski katika ngazi ya klabu na timu ya taifa msimu huu imechangiwa na mabao manne ya UEFA aliyofunga ugenini dhidi ya Red Star Belgrade mnamo Novemba 26, 2019, kabla ya kujaza kimiani magoli manne katika Ligi Kuu ya Bundesliga dhidi ya Schalke mnamo Agosti 24.

Alifungia Poland mabao matatu katika mechi ya kufuzu kwa fainali za Euro iliyowakutanisha na Latvia ugenini mnamo Oktoba 10.

Katika kipindi cha misimu miwili iliyopita, Lewandowski anajivunia kufungia Bayern jumla ya mabao 67 katika mapambano yote, rekodi yake ikikaribia sasa ile ya Messi ambaye amefungia Barcelona jumla ya magoli 95 kwenye mashindano yote katika misimu miwili iliyopita.