Michezo

Homeboyz kusajili wanaraga watano wa haiba kubwa kwa minajili ya msimu ujao wa Kenya Cup

August 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Homeboyz RFC kinatazamia kusajili wanaraga watano kadri wanavyopania kuimarisha zaidi kikosi chao kwa minajili ya kampeni za msimu ujao.

Mwenyekiti Mike Rabar amesema hatua yao inachochewa kiu ya kujitwalia taji la Ligi Kuu ya Kenya Cup msimu ujao kutokana na ari inayowatawala kwa sasa baada ya kukamilisha kampeni za muhula huu katika nafasi ya tatu.

Hadi msimu wa raga ya humu nchini ulipositishwa Aprili 2020 kutokana na janga la corona, Homeboyz walikuwa wakijiandaa kuvaana na Menengai Oilers kwenye mchujo na mshindi angejikatia tiketi ya kuvaana na mabingwa watetezi, KCB.

“Ingawa tulikuwa na kampeni bora katika msimu wa 2019-20, hatukuridhika na matokeo tuliyosajili. Hii ndiyo sababu ambayo imetuchochea kujinasia huduma za wachezaji wapya ili kuleta nguvu mpya itakayotutambisha zaidi,” akasema Rabar.

Homeboyz almaarufu ‘The Deejays’ walijizolea jumla ya alama 66 msimu huu na wakafaulu kuwaangusha viongozi Kabras RFC kwa 20-17 kabla ya kuwalazimishia mabingwa KCB sare ya 24-24.

Kufikia sasa, Homebyz tayari wamepoteza huduma za mwanaraga Mark Wandetto ambaye amejiunga na Kenya Harlequins.

Harlequins ambao pia wamejinasia huduma za Leroy Mbugua wa Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta, wamewakweza chipukizi Boniface Ochieng, Elisha Koronya na Melvin Thairu waliokuwa tegemeo kubwa la timu ya taifa ya wachezaji 15 kila upande, Kenya Simbas mnamo 2019 hadi kikosi cha kwanza.

Katika kivumbi cha msimu huu, Harlequins walisajili ushindi katika mechi tano na kupoteza jumla ya michuano 11 katika matokeo yaliyowashuhudia wakijizolea alama 28 pekee.