Habari

Serikali yapuuza raia ng'ambo

August 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na DOUGLAS MUTUA

SERIKALI ya Kenya inaendelea kupata fedheha na lawama kwa kuwapuuza wananchi wake wanaoishi nje ya nchi, hasa wanapohitaji kusaidiwa kwa dharura.

Mwanahabari Yassin Juma, ambaye amekaa jela nchini Ethiopia kwa miezi kadhaa bila Serikali ya Kenya kuingilia kumwokoa, sasa ameambukizwa ugonjwa wa Covid-19 akiwa seli, wakili wake Kedir Bullo amesema.

Hayo yanajiri wakati ambao mamia ya Wakenya wamekwama nchini Lebanon baada ya kuathiriwa na mlipuko uliotokea wiki iliyopita jijini Beirut.

Wakenya hao, ambao sasa wanaishi barabarani, wameachwa mikononi mwa raia wa Lebanon wasiowajali, ambao wameajiriwa na serikali ya Kenya.

Wakenya hao wamekuwa wakiililia serikali na hususan Rais Uhuru Kenyatta awasaidie kurejea nyumbani kwa sababu hawana nauli za ndege.

Juzi Wakenya hao walipoandamana nje ya ubalozi mdogo wa Kenya jijini Beirut, mmoja wa maafisa wanaousimamia alitoka nje, akafunga mlango kwa fujo na kuwaambia: “Andamaneni usiku kucha, mimi naenda kulala!”

Tamko hilo halikuwashangaza wengi wanaoishi Lebanon kwa sababu wasimamizi wa ubalozi huo wana sifa za kuwatusi na hata kuwapiga Wakenya wanaotafuta msaada hapo.

Ubalozi huo unaendeshwa na wakili kwa jina Sayed Chalouhi, akisaidiwa na Bw Kassem Jaber. Mkuu wao ni balozi wa Kenya nchini Kuwait, Bi Halima Mohamud.

Hii ina maana kwamba Kenya haina maafisa wa kibalozi nchini Lebanon wenye asili ya Kenya, hivyo maslahi yao hayashughulikiwi ipasavyo.

Bi Halima juzi alitoa taarifa akiwa Kuwait na kuwaambia Wakenya walio Lebanon wajitafutie njia zao kibinafsi za kurudi Kenya au waombe vibali vya dharura ili wasaidiwe kwa sababu haijulikani wamekuwa wakifanya nini huko.

“Ubalozi huu umegundua kwa masikitiko makubwa kwamba ajira na hali za uhamiaji za Wakenya kadhaa walioandamana nje ya ubalozi mdogo nchini Lebanon hazijulikani,” sehemu ya taarifa yake ilisema.

Kisa cha Bw Juma kuzuiliwa Ethiopia na kile cha raia wa Kenya kukwama Lebanon ni mifano ya majuzi tu ya uozo ambao umekolea kwenye Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Kenya, hasa kuwahusu raia walio ng’ambo.

Visa vingi vimeripotiwa ambapo jamaa na marafiki wa watu wanaofanya kazi nchini Saudi Arabia na Mashariki ya Kati kwa jumla wameililia Serikali iwasaidie kurejesha watu wao nyumbani bila mafanikio.

Katika mojawapo ya video iliyotoka Saudia, Wakenya wanaonekana wakimshikilia mwanamke ambaye yuko hali mahututi.

Wanasema walikwenda huko kufanya kazi za nyumbani na shambani, lakini janga la corona limewakosesha ajira na sasa wanaishi maisha ya taabu, bila chakula wala makao salama.

“Baadhi yetu wameishia kuishi mitaani au kwenye vituo vya petroli. Tunateswa na kubaguliwa kwa misingi ya rangi,” mmoja wa wanaozungumza kwenye video hiyo anasema.

Ni baada ya Wakenya kupigwa hadi kufa, wengine kutupwa hadi kutoka juu ya ghorofa na kuvunjikavunjika sehemu za mwili au hata kufa ambapo Kenya iliwapiga marufuku mawakala waliokuwa wakisafirisha wafanyakazi wa nyumbani hadi Jordan mnamo 2015.

Hata hivyo, marufuku hiyo iliondolewa kimyakimya baada ya mashirika mengi, hasa yanayomilikiwa na raia wa Jordan, kuilalamikia serikali ya Kenya.

Mpaka sasa watu wanauawa, serikali iko kimya, na Wajordan wanaendeleza biashara ya utumwa wa kisasa bila kuzuiwa na yeyote. Malipo huko ni duni, na wakati mwingine mtu halipwi ng’o!

Wuhan

Itakumbukwa Wakenya waliokuwa mjini Wuhan nchini China waliililia serikali ya Kenya wakitaka iwarejeshe nyumbani tangu Januari hadi Mei mwaka huu wakati ambapo ugonjwa wa Covid-19 ulichacha zaidi huko.

Balozi wa Kenya nchini humo, Bi Sarah Serem, aliwaambia waliotaka kurejea nyumbani ni sharti wangejilipia jumla ya Sh80,000.

Hali ni hii ya kukatisha tamaa pia ipo kwenye balozi za Kenya zilizo kwenye mataifa yaliyostawi ukiwemo Ubalozi wa Kenya Marekani.

Wakenya wanaokwenda pale kwa shughuli rasmi kama vile kuchukua paspoti au vitambulishio vipya hawahudumiwi kwa wakati bila kutoa hongo, au kujuana na maafisa wanaofanya kazi pale.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia haya ubalozini hapo mwaka jana Serikali ya Kenya ilipokuwa ikisajili watu kwa ajili ya Huduma Namba.

Wakenya waliotoa hongo walikuwa wakihudumiwa haraka baada ya nusu saa pekee ilhali waliokataa kutoa chochote waliketi mchana kutwa na hata baadhi yao wakaambiwa warejee siku iliyofuata.

Palikuwepo na ‘mabroka’ ambao walikuwa wakiwalaki watu mlangoni na kuwauliza iwapo walihitaji kuondoka haraka, na jibu likiwa ndio, basi mchakato mzima wa kutoa na kupokea hongo kwa ajili ya huduma rasmi za serikali ulianza!

Balozi wa Kenya nchini Amerika huwa amezingirwa na watu wajanja, maafisa wa kibalozi na malofa wengine wanaokuwa pale kwa ajili ya ‘kuungaisha’ watu na balozi mwenyewe. Malalamiko kama hayo pia yanatokea nchini Uingereza.