Akumu afungua akaunti ya mabao nchini Afrika Kusini huku Olunga akiongoza jedwali la wafungaji bora katika Ligi Kuu ya Japan
Na CHRIS ADUNGO
KIUNGO Anthony Akumu wa Harambee Stars alifungua rasmi akaunti yake ya mabao kambini mwa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Hii ni baada ya nyota huyo wa zamani wa Gor Mahia na Zesco United ya Zambia kufunga goli na kusaidia waajiri wake kutoka nyuma na kuwapokeza Polokwane City kichapo cha 3-2 katika Ligi Kuu ya PSL.
Polokwane walijiweka uongozini katika dakika ya 17 kupitia kwa Nku kabla ya Maluleke kufanya mambo kuwa 2-0 mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Ingawa hivyo, Katsande aliwarejesha Chiefs mchezoni katika dakika ya 71 baada ya kushirikiana vilivyo na Nurkovic aliyechangia pia bao la pili lililofumwa wavuni na Akumu kunako dakika ya 75. Bao la tatu la Chiefs lilijazwa kimiani na Nurkovic mwishoni mwa kipindi cha pili.
Ushindi huo uliwakweza Chiefs hadi kileleni mwa jedwali kwa alama 52 baada ya mechi 24 za hadi kufikia sasa ligini msimu huu. Miamba hao kwa sasa wanajivunia pengo la alama sita kati yao na Mamelowdi Sundowns wanaoshikilia nafasi ya pili.
Kwingineko, fowadi matata wa Harambee Stars Michael Olunga, aliendeleza ubabe wake katika Ligi Kuu ya Japan msimu huu kwa kufungia waajiri wake Kashiwa Reysol bao lake la 11 hadi kufikia sasa.
Hata hivyo, goli lake hilo halikuwezesha Reysol kujikwamua kwenye meno ya Cerezo Osaka waliowang’ata 3-1.
Bruno Mendes, Koga Nishikawa waliwapa Osaka uongozi wa mapema wa 3-0 kabla ya Olunga kuwafutia waajiri wake machozi na kudhibiti kabisa jedwali la wafungaji bora kwenye Ligi Kuu ya Japan (J1 League).
Kwingineko, aliyekuwa kipa chaguo la kwanza la Harambee Stars, Arnold Origi, alionyeshwa kadi nyekundu katika mechi iliyoshuhudia waajiri wake HIFK wakipepetwa 3-2 na Inter Turku kwenye Ligi Kuu ya Finland.
Origi alionyeshwa kadi ya kwanza ya manjano kunako dakika ya 87 kabla ya kuonyeshwa ya pili dakika mbili baadaye. Awali, kipa huyo wa zamani wa Lillestrom nchini Norway, alikuwa amesababisha penalti mbili zilizofungwa na Turku kwenye mechi hiyo.