• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Ishara uchaguzi mkuu wa FKF utacheleweshwa hata zaidi

Ishara uchaguzi mkuu wa FKF utacheleweshwa hata zaidi

Na CHRIS ADUNGO

MIPANGO ya kuandaliwa kwa uchaguzi wa viongozi wapya wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) hivi karibuni huenda ikacheleweshwa zaidi.

Hii ni baada ya wawaniaji wanane wa kiti cha urais kutaka Jopo la Mizozo ya Spoti (SDT) kusitisha shughuli hiyo ambayo tayari imetupiliwa mbali na jopo hilo chini ya mwenyekiti John Ohaga mara mbili katika kipindi cha miezi minane iliyopita.

Uchaguzi huo uliahirishwa kwa mara ya kwanza mnamo Desemba 2019 kisha Machi 2020 kutokana na ukiukwaji wa baadhi ya Sheria za Michezo nchini Kenya za mwaka wa 2013.

Sita hao ambao wamewasilisha kesi kwa SDT ni Sam Nyamweya, Alex Ole Magelo, Steve Mburu, Twaha Mbarak, Lordvick Aduda na Nicholas Musonye ambao wanapigania fursa ya kumshinda na hivyo kurithi nafasi ya Rais wa sasa wa FKF, Nick Mwendwa.

“Wakati umefika kwa FKF kufuata sheria. Klabu zote zinastahili kukubaliwa kupiga kura katika uchaguzi huo na mchakato wa kuamua nani asiyestahili kushiriki kuwekwa wazi kwa wadau wote. Hilo likifanyika, basi tutakuwa radhi kushiriki uchaguzi huo hata kesho,” akasema Nyamweya.

Wengine ambao wamewasilisha malalamiko yao kwa SDT ni Angeline Mwikali anayelenga kuhifadhi kiti cha uanachama wa Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ya FKF katika eneo la Mashariki na Michael Esakwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa FKF wakati Nyamweya alipokuwa mwenyekiti wa shirikisho hilo kati ya 2011 na 2015. SDT itasikiliza na kuamua kesi hiyo hapo kesho.

Kwa pamoja na wawakilishi wa klabu za Bondeni na Cheptiret, wanane hao wameishtaki Bodi ya Uchaguzi ya FKF, mwenyekiti wake Kentice Tikolo na FKF yenyewe, na wanaitaka SDT kutupilia mbali mwongozo wa uchaguzi uliotolewa na Bodi ya Uchaguzi ya FKF mwanzoni mwa wiki iliyopita.

“Tunahisi kwamba FKF haiwezi kuandaa uchaguzi wa haki kwa sababu hakuna usawa kwa wagombezi na hata wapigakura kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa majuzi. Isitoshe, mwongozo huo unahitilafiana na Katiba ya Kenya na maamuzi ya awali ya SDT,” akasema Nyamweya.

Malalamishi mengine dhidi ya FKF yamewasilishwa na wadau mbalimbali wa soka katika mahakama tofauti za Mombasa, Murang’a, Kericho na Nairobi.

Mnamo Jumanne iliyopita, Tikolo alitangaza kwamba uchaguzi mpya wa FKF ungefanyika Septemba 19 katika kiwango cha kaunti huku wa ule wa kitaifa ukiandaliwa Oktoba 17, 2020. Bodi hiyo ilichapisha majina ya klabu zitakazokubaliwa kupiga kura mnamo Agosti 12. Ilitenga Agosti 17-18 kusikiza malalamishi yoyote kuhusu orodha hiyo ya wapigakura.

Rufaa zozote kuhusu orodha ya klabu zitakazoshiriki kura zitasikilizwa na kuamuliwa na kamati ya rufaa Agosti 19-21. Orodha ya mwisho ya wapigakura kisha itachapishwa Agosti 22 na wagombeaji wanaomezea viti vya kaunti kuwasilisha fomu zao Agosti 25-26.

Orodha ya kwanza ya wawaniaji wa viti kwenye kaunti itachapishwa Agosti 29, huku wagombeaji wa urais wa FKF wakihitajika kuwasilisha fomu za wadhifa huo kufikia Agosti 31.

You can share this post!

Watford sasa wapata kocha mrithi wa Pearson

Kevin Opiyo Oliech aaga dunia, marehemu ni kaka yake Dennis...