Michezo

Inter yainyeshea Donetsk matano UEFA

August 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

ROMELU Lukaku na Lautari Martinez walifunga mabao mawili kila mmoja na kusaidia Inter Milan ya Italia kuwaponda Shakhtar Donetsk kutoka Ukraine 5-0 kwenye nusu-fainali ya Europa League msimu huu.

Ushindi kwa Inter kwenye mechi hiyo iliyochezewa mjini Dusseldorf, Ujerumani mnamo Agosti 17, 2020 uliwakatia tiketi ya Europa ambayo kwa sasa itawakutanisha na mabingwa mara tano, Sevilla mnamo Agosti 21 mjini Cologne, Ujerumani.

Martinez aliwafungulia Inter ukurasa wa mabao kunako dakika ya 19 baada ya kukamilisha kwa kichwa krosi aliyomegemewa na Nicolo Barella ambaye alichuma nafuu kutokana na masihara ya kipa wa Shakhtar, Andriy Pyatov.

Danilo D’Ambrosio alifunga bao la pili la Inter kupitia kona iliyochanjwa na Marcelo Brozovic katika dakika ya 64.

Martinez ambaye anahusishwa pakubwa na Barcelona, alipachika wavuni bao la tatu la Inter katika dakika ya 74 kabla ya Lukaku kuzamisha kabisa chombo cha wapinzani wao hao kwa mabao mawili ya haraka mwishoni mwa kipindi cha pili.

Lukaku ambaye ni mchezaji wa zamani wa Everton na Manchester United, kwa sasa anajivunia rekodi ya kufunga katika jumla ya mechi 10 mfululizo za Europa League na amepachika wavuni jumla ya mabao 33 hadi kufikia sasa msimu huu.

Fursa ya pekee kwa Shakhtar kutatiza ngome ya Inter ilikuwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza ambapo Junior Moraes alisalia uso kwa macho na kipa Samir Handanovic aliyedhibiti vilivyo kombora aliloelekezewa.

Baada ya kukosa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwa pointi moja, Inter kwa sasa wana fursa maridhawa ya kutia kapuni taji la kwanza tangu 2011 watakaposhuka dimbani mnamo Ijumaa kuvaana na masogora wa kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uhispania na klabu ya Real Madrid, Julen Lopetegui.

Chini ya kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte, Inter wanajivunia kwa sasa ufufuo mkubwa. Mara ya mwisho kwa Inter kunyanyua kombe ni miaka tisa iliyopita ambapo walitawazwa mabingwa wa Kombe la Dunia na Coppa Italia mnamo 2010-11.

Conte ambaye alipigwa kalamu na Chelsea mnamo Julai 2018, amepania kuamsha Inter kwa kutegemea huduma za wanasoka ambao kwa sasa ni mawe ya pembeni yaliyokataliwa na waajiri wao wa zamani. Hao ni Lukaku, Alexis Sanchez na Ashley Young waliotemwa na Manchester United, kiungo Christian Eriksen aliyetokea Tottenham Hotspur na fowadi Victor Moses ambaye kwa sasa anawachezea kwa mkopo kutoka Chelsea.

Lukaku amehusika katika mabao 18 ambayo yamefungwa na Inter kwenye mechi 10 zilizopita za Europa League. Amefunga magoli 14 na kuchangia mengine manne.

Iwapo Lukaku atafunga bao jingine kwenye fainali dhidi ya Sevilla, basi atafikia rekodi ya aliyekuwa mwanasoka matata wa timu ya taifa ya Brazil, Ronaldo, aliyefunga jumla ya mabao 34 akivalia jezi za Inter mnamo 1997-98.

Shakhtar ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Ukraine, walitinga nusu-fainali za Europa League msimu huu baada ya kuwabandua Benfica ya Ureno, Wolfsburg ya Ujerumani na FC Basel kutoka Uswisi. Hadi walipopepetwa na Inter, Shakhtar hawakuwa wamepoteza mechi yoyote kati ya 11 za awali.

Inter kwa sasa wanaingia fainali ya 10 katika soka ya bara Ulaya wakijivunia rekodi ya kutoshindwa katika jumla ya michuano 11 iliyopita.

Kichapo cha 5-0 ambacho Inter walipokeza Shakhtar ndicho kinono zaidi kuwahi kusajiliwa kwenye mchuano wa mkondo mmoja wa nusu-fainali za UEFA Cup au Europa League.

Ni mara ya kwanza kwa Shakhtar kubebeshwa idadi kubwa zaidi ya mabao katika soka ya bara Ulaya tangu kikosi hicho kitandikwe 6-0 na Manchester City kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya mnamo Novemba 2018.

Inter wameibuka washindi katika jumla ya mechi tano mfululizo za soka ya bara Ulaya (mechi za kufuzu zisipokuwemo) kwa mara ya kwanza tangu Aprili 2010 ambapo walishinda jumla ya mechi sita mfululizo kuanzia Disemba 2009 na hivyo kutinga fainali ya UEFA.

Martinez na Lukaku ndio wanasoka wa kwanza kufungia Inter zaidi ya mabao 20 kwenye kampeni za msimu mmoja tangu Adriano na Obafemi Martins afanye hivyo mnamo 2004-05.

Lukaku ambaye ni mzawa wa Ubelgiji, kwa sasa ndiye mwanasoka wa kwanza kutoka Serie A msimu huu kuwajibishwa katika mechi 50 kwenye mapambano yote na ndiye mchezaji wa kwanza wa Inter kuwahi kufanya hivyo tangu Samuel Eto’o (53) na Javier Zanetti (52) mnamo 2010-11.