Madhila ya wajane na watoto wanaopasua mawe Nyamira
Na STEVE MOKAYA
Huku makali ya kudorora kwa uchumi kutokana na gonjwa la COVID-19 yakizidi kuwakeketa watu wengi humu nchini, baadhi ya wajane na watoto kutoka Kaunti ya Nyamira wamegeukia kupasua na kuuza mawe ili kupata riziki.
Wanawake hao kutoka katika eneo la Gekomu,wadi ya Kemera, wamekuwa wakiifanya kazi hii kwa muda mrefu sasa; ila kwa watoto, kufungwa kwa shule na ukosefu wa chakula nyumbani kumewafanya kujitosa kwenye ulingo huo.
Hyline Kwamboka amefanya kazi hii tangu mwaka wa elfu mbili na saba, wakati bwana wake aliaga dunia. Anasimulia jinsi ugumu wa maisha, na ukosefu wa kazi ya kutegemewa ulivyomlazimisha kuanza kupasua mawe.
“Bwanangu aliaga dunia na kuniacha na watoto saba. Sikuwa na kazi rasmi ya kufanya, na watoto lazima wangesomeshwa,na pia chakula kipatikane nyumbani. Sikuwa na budi ila kuinua nyundo kupasua mawe,” anasema.
Tangu mwaka huo wa elfu mbili na saba, Kwamboka ameyashuhudia mafanikio kutokana na kazi hii.
“Nimewasomesha watoto wangu kutokanana kazi hii. Wengine wako katika shule za upili na wengine katika vyuo anuwai,” anasema.
Hata hivyo, anasema kuwa kazi hii ina madhila yake kabambe, na kuwa inahitaji uvumilivu wa aina yake.
“Shida kubwa katika kazi hii ni majeraha. Wakati mwingine mawe haya huniumiza sana, hadi ninaenda hospitalini kushonwa. Hata hivyo, ninavumilia na baada ya kupona ninarudi na kuendelea kama kawaida,” anasema.
Kwamboka anafanya kazi hii na binti wake kifungua mimba, Vinic Kerubo. Kerubo aliachia shule katika kidato cha pili, baada ya babaye kuaga dunia, na hivyo karo ikawa mzigo. Kutokana na hali hiyo, alilazimika kuzamia kazi hii ili asaidie mamaye kuiinua familia yao.
“Wajua mimi ndiye mkubwa na ni lazima nisaidie mama. Tunategemea kazi hii kupata riziki. Hapa pia ndipo tupatapo karo kwa ndugu zangu wadogo,” anasema.
Hata hivyo, anaongeza kuwa kazi hii si ya kufurahisha kamwe, maadam changamoto zake ni za kuatua moyo.
“Saa nyingine unagonga ,mawe kwa muda mrefu na hayapasuki. Unaweza kuchukua hata wiki nzima kujaza gari moja, na nyumbani kuna njaa,” anasema.
Mawe ya kina mama hawa aghalabu hununuliwa na wajenzi wa nyumba, lakini kuja kwao si kwa kutegemewa. Mbali na hilo, bei yao ni ya chini, ikilinganishwa na kazi nzito waifanyao, na kwa muda mrefu. Wanaeleza kuwa bei inaazia shilingi elfu moja na mia tano hadi elfu tatu, kutegeme na uelewano kati ya mnunuzi na mwuzaji.
Katika eneo hili, ardhi imejaa mawe na changarawe karibu kila mahali, na hivyo kufanya upanzi wa chakula kuwa kugumu. Kwa wale wanaojaribu kufanya kilimo cha mimea katika eneo hili, inawabidi kwanza kutoa mawe na changarawe, ili angaa wafikie udongo wenye rutuba kidogo.
Getrude Kerubo ni mmoja wao na anasema kuwa hiyo ndiyo sababu kuu ya kumfanya afanye biashara hii ya mawe.
“Huku kwetu chakula hakikiui vizuri. Ardhi hii ni mbaya, hata upande kwa kutumia mbolea nyingi, bado mazao ni mabaya. Hivyo huwezi kutegemea kilimo cha shambani kupata chakula,” anasema.
Anazidi kusema kuwa zile siku ambazo riziki ya mawe inafeli, inambidi akafanye kazi za vibarua katika miji ya watu kama vile kuchuna chai, ili apate mkate wa siku.
Mbali na kina mama,wapo watoto pia. Wengi wao ni wadogo, wakiwa katika shule za msingi na wachache katika shule za upili. Wamejaa miongoni mwa kina mama hawa. Brian Kebago ni mmoja wao. Kebago yuko katika kidato cha tatu katika shule ya upili ya mseto ya Ekerubo.
“Hakuna pesa nyumbani na wazazi hawajiwezi. Isitoshe, shule zimefungwa na hivyo hakuna masomo. Kwa vile mimi si kilema na tunahitaji pesa, hasa za chakula, inanibidi nije hapa nifanye kazi,” anasema.
Kebago anasema kuwa pesa apatazo kutokana na kazi hii anatumia kununua bidhaa za kimsingi nyumbani. Nyingine anatumia kujinunulia mavazi. Hata hivyo, anasema kuwa hangependa wanafunzi wenzake kujua kuwa anafanya kazi hii.
“Sitaki hata wajue, kwa sababu wakijua wataanza kunichongoa na kunidhihaki tukiwa shuleni,” anasema.
La ajabu ni kuwa wanaume wa sehemu hii wanadharau kazi hii na kuichukia pia. Charles Barongo ni mkazi wa hapa na anaeleza sababu ya hali hiyo.
“Wanaume wengi wanapenda pesa za haraka haraka. Wanapenda kuenda katika vibarua na kulipwa kila siku. Wanaona kuwa kuja hapa kugongagonga mawe kisha wangoje pesa kwa muda mrefu ni shida,” anasema.