Michezo

Sevilla yapiga Inter kutwaa Europa kwa mara ya 6

August 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MIAMBA wa soka nchini Uhispania, Sevilla waliweka rekodi ya kutawazwa mabingwa wa Europa League kwa mara ya sita baada ya kupepeta Inter Milan ya Italia 3-2 kwenye fainali iliyowakutanisha mjini Cologne, Ujerumani mnamo Ijumaa.

Mechi hiyo ilianza kwa Romelu Lukaku kutikisa nyavu kabla ya nyota huyo wa zamani wa Everton na Manchester United kujifunga mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kushindwa kudhibiti mpira uliopigwa na beki Diego Carlos aliyesababisha penalti iliyofungwa na Lukaku.

Ina maana kwamba Inter ya kocha Antonio Conte itasubiri zaidi kabla ya kujinyanyulia taji la kwanza ambalo wamekuwa wakilisaka kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Bao la Lukaku lilikuwa lake la 34 msimu huu. Ni ufanisi uliomfanya kuwa mwanasoka wa kwanza kuwahi kufunga katika jumla ya mechi 11 mfululizo za Europa League. Mabao mengine ya Sevilla yalifungwa na Luuk de Jong kupitia krosi za Jesus Navas na Ever Banega kabla ya beki Diego Godin kufungia Inter katika dakika ya 35.

Kwa kocha Julen Lopetegui wa Sevilla, hilo lilikuwa taji lake la kwanza kutwaa tangu apokezwe mikoba ya kikosi hicho ambacho kwa sasa hakijapoteza mechi yoyote kati ya 21 zilizopita tangu Februari mwaka huu.

“Kikosi kimedhihirishwa kwamba wao ni wafalme wa soka ya bara Ulaya. Tumewapa mashabiki wetu sababu nyingine ya kusherehekea popote walipo,” akatanguliza kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uhispania.

“Hata iwapo tungepoteza mechi hii dhidi ya Inter, sidhani tungenung’unika. Vijana walicheza vyema na kuridhisha tangu mwanzoni mwa msimu. Bahati ilisimama nasi na juhudi zetu kutuzwa,” akaongeza.

Mataji tisa yaliyopita katika soka ya Europa League yamenyakuliwa na vikosi kutoka Uhispania na Uingereza. Sevilla wametwaa ubingwa wa kivumbi hicho mara nne, Chelsea mara mbili kisha Atletico Madrid na Manchester United mara moja kila mmoja. Parma ndicho kikosi cha mwisho cha Italia kutwaa ufalme wa Europa League mnamo 1999.

Kwa kuwakung’uta Inter, Sevilla waliendeleza rekodi nzuri ya kutowahi kupoteza mechi katika fainali ya Uefa Cup au Europa League katika kipindi cha miaka sita iliyopita. Hata hivyo, kikosi kilichotegemewa na Lopetegui kilikuwa kipya kabisa na hakuna mwanasoka yeyote aliyekuwa sehemu ya timu iliyonyanyua mataji ya Europa League kwa misimu mitatu mfululizo kati ya 2014 na 2016.

Lopetegui ambaye alipokezwa mikoba ya Sevilla mwanzoni mwa msimu huu, alikisuka kikosi kipya na wanasoka tisa kati ya 11 waliounga kikosi cha kwanza mjini Cologne walikuwa wakinogesha msimu wao wa kwanza ndani ya jezi za Sevilla.

Kila walipogusa mpira, wachezaji wa Sevilla walishangiliwa na mashabiki wawili waliosafiri nao baada ya maafisa wawili katika kikosi cha watu 25 kilichosafiri Ujerumani kujinyima na kutoa tiketi zao kwa mashabiki wenye nambari za usajili 2108 na 2020 (kuashiria tarehe ya kupigwa kwa fainali hiyo).

Chini ya Conte aliyesajili wanasoka watano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika msimu wake wa kwanza uwanjani San Siro, Inter wamefufua makali yao kiasi kwamba waliambulia nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu huu.

Hiyo ilikuwa nafasi nzuri zaidi kuwahi kushikiliwa na Inter kwenye jedwali la Serie A tangu 2010-11. Huo ndio ulikuwa msimu wao wa mwisho kujinyanyulia taji baada ya kuwazidi Palermo maarifa uwanjani Olimpico, Roma.

Beki Ashley Young wa Inter aliweka historia ya kuwa mwanasoka wa kwanza mzawa wa Uingereza tangu 2001 kunogesha fainali ya soka ya soka ya bara Ulaya akivalia jezi za kikosi kisicho cha EPL. Owen Hargreaves alichezea Bayern Munich kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2001.

Inter walipoteza fainali yao ya kwanza kwenye soka ya bara Ulaya tangu 1997 walipozidiwa ujanja na Schalke kupitia penalti kwenye Uefa Cup.

Tangu msimu wa 2009-10, taji la Europa League limenyanyuliwa na kocha mzawa wa Uhispania katika fainali sita kati ya 11. Unai Emery alitwaa ubingwa huo mara tatu kisha Quique Sanchez Flores, Rafael Benitez na Lopetegui mara moja kila mmoja.