Habari

Wauzaji wa mitumba wapewa eneo kunyunyuzia bidhaa dawa

August 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na ANTHONY KITIMO

SERIKALI imeanza kutenga maeneo mawili yatakayotumika kunyunyuzia nguo na viatu vya mitumba vitakapoanza kuingizwa nchini.

Maeneo hayo yatakuwa na mabohari mawili maalum, ambapo bidhaa hizo zitanyunyiziwa dawa ili kuuwa virusi vyovyote vya corona ambavyo huenda vitakuwa.

Tayari, Halmashauri ya Kukadiria Ubora wa Bidhaa (KEBS), imetenga maeneo maalum ya kunyunyizia mizigo hiyo katika Bandari ya Mombasa, na depo ya kupokea shehena ya Nairobi.

Hatua hiyo ni sehemu ya kanuni ambazo wauzaji mitumba watatakiwa wazingatie, wakati huu ambapo serikali imewaruhusu kuanza upya biashara hiyo.

kanuni hizo ni za kuhakikisha kuwa wahudumu zaidi ya 35,000 wanohusika kwenye uingizaji mitumba nchini hawaambukizwi virusi vya Corona, ambavyo kawaida hukaa katika nguo kwa hadi saa 72 (siku tatu).

Kwa mujibu wa kanuni hizo, wahudumu hao watalazimika kujisajili kwa KEBS.

Vile vile, lazima nguo na viatu vyote zikaguliwe na kupewa kibali maalum kabla yao kuruhusiwa kuzisafirisha katika maeneo mbalimbali nchini.

Wahudumu pia watalazimika kuziambia idara husika kuhusu nchi na mahali maalum wanakotoa mizigo yao.

Kulingana na Waziri wa Biashara na Viwanda, Bi Betty Maina, mizigo yote inayoingizwa nchini lazima iwe na vyeti maalum kutoka nchi ilikoagizwa kuonyesha imenyunyiziwa dawa na kuoshwa.

“Lazima kila mzigo uwe umewekwa kwenye karatasi ya wazi na ambayo haipenyezi maji. Sharti pia iwe na cheti maalum kutoka nchi husika kuonyesha imetimiza viwango vyote vinavyohitajika ili kutangazwa kuwa salama kusafirishwa,” akasema waziri, kwenye kanuni alizotoa wiki iliyopita.

Mizigo ya wale ambao hawatazingatia kanuni hizo itakataliwa, huku wamiliki wake wakiwa kwenye hatari kuchukuliwa hatua za kisheria.