Rais akiuka ahadi ya kutii sheria
MWANGI MUIRURI NA BENSON MATHEKA
HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kupuuza uamuzi wa mahakama kuhusu utoaji wa hatimiliki za ardhi ya kampuni ya Embakasi Ranching wiki iliyopita, inakiuka ahadi aliyotoa alipoapishwa 2017 kuwa ataheshimu utawala wa sheria na matawi mengine ya serikali.
Hiki ni kisa cha majuzi kabisa kwa serikali kupuuza maagizo ya korti, hatua ambayo imetajwa kuwa hatari kwa utawala wa kisheria.
Kwenye hotuba yake alipoapishwa Novemba 28, 2017, Rais alisisitiza umuhimu wa wananchi wote kutii utawala wa sheria, ambapo aliahidi serikali yake itakuwa mstari wa mbele.
“… Sheria lazima iwe kilele na kimbilio kwa kila Mkenya. Hakuna yeyote kati yetu anayepasa kuvunja sheria, ama utaratibu wa Katiba… Wakati korti ya kigeni ya ICC ilipohitaji tutii maagizo yake tulifanya hivyo… Mahakama ya Juu ilipofuta ushindi wetu tulitii…
“Utawala wangu umeonyesha kwa vitendo kwa uko tayari kutii na kuongoza kwa utawala wa sheria. Kwa hivyo tunatarajia hali sawa kutoka kwa kila mwananchi.
“Katiba yetu imebuni matawi matatu huru ya serikali… Kama Rais nitatekeleza wajibu wangu kama ilivyoelezwa kwenye Katiba. Natarajia matawi mengine ya serikali kufanya hivyo pia. Ni lazima kila mtu afanye kazi yake kulingana na Katiba.
“… Hatupaswi kuharibu taasisi zetu kila mara zinapokosa kutimiza matakwa yetu. Hata kama utawala wa sheria hautatui matatizo yetu papo kwa hapo, utiifu kwa sheria unabakia kuwa hakikisho pekee la haki,” akasema Rais Kenyatta.
Kwa muda sasa serikali imeshutumiwa hasa kwa kukiuka maagizo ya mahakama pamoja na kuingilia utendakazi wa Mahakama na Bunge, mambo ambayo Rais Kenyatta aliahidi kuzingatia.
Lakini wengine wanasema baadhi ya maamuzi ya mahakama yanatatiza shughuli za maendeleo na hivyo hayana budi kupuuzwa.
“Nyakati zingine mambo yanafaa kuharakishwa ili kuepukana na vizingiti ambavyo huwekwa na wanaojifanya kuwa watetezi wa wanyonge ilhali wanajifaidi wenyewe,” akasema Katibu wa Wizara ya Ardhi, Nicholas Muraguri.
Aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Embakasi Ranch, Nyokabi Mathenge pia aliunga mkono hatua hiyo akisema Rais Kenyatta alichukua hatua iliyowafaa wenyehisa, kwani hali ilivyo katika mradi huo ni tata na ilihitaji maamuzi ya kipekee.
Katibu wa Wizara ya Usalama, Karanja Kibicho naye amekuwa akizilaumu korti akidai hazisaidii serikali kwenye vita dhidi ya pombe haramu kutokana na maamuzi zinayotoa kama vile faini ya chini na kuachilia washukiwa.
Lakini Wakili John Khaminwa ameonya kuwa mwelekeo huo ni hatari kwa utawala wa sheria, ambao Rais Kenyatta aliambia taifa na ulimwengu mnamo Novemba 28, 2017 kuwa atazingatia.
“Taifa hustawi wakati sheria inapoheshimiwa na wananchi wote zikiwemo idara za serikali,” akasema Bw Khaminwa kwenye barua kwa Dkt Muraguri kuhusu agizo la kusitisha utoaji hati za Embakasi Ranching.
Rais Uhuru Kenyatta pia amekataa kuapisha majaji 41 licha ya mahakama kumwagiza mara mbili kufanya hivyo.
Julai 2020 aliteua mawakili wakuu licha ya agizo la korti kusitisha uteuzi wao.
Upuuzaji huo umekita mizizi serikalini, ambapo mnamo Mei mwaka huu Serikali ilipuuza agizo lililozuia ubomoaji makazi mtaani Kariobangi jijini Nairobi.
Mnamo Aprili 2020 Serikali ilipuuza agizo la mahakama na kubomoa vibanda vya kupulizia dawa wakazi wa Nairobi zilizowekwa na Gavana Mike Sonko.
Serikali pia imesita kuwafidia watu waliodhulumiwa licha ya kuagizwa na mahakama kuwalipa.
Tangu 2018, maafisa wakuu wa serikali wamekataa kumrudishia wakili Miguna Miguna paspoti yake, licha ya korti kuwaagiza.
Serikali pia imeshutumiwa kwa kuingilia uhuru wa Bunge la Kitaifa na lile la Seneti.