• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 1:08 PM
ODONGO: Marais Afrika wajue mamlaka yako mikononi mwa raia

ODONGO: Marais Afrika wajue mamlaka yako mikononi mwa raia

Na CECIL ODONGO

VIONGOZI barani Afrika wanafaa kufahamu kwamba mamlaka yanashikiliwa na raia kabla ya wanajeshi kuingilia na kutekeleza mapinduzi mara kwa mara jinsi ilivyofanyika nchini Mali wiki jana.

Marais walioko mamlakani hawafai kukwamilia uongozini hata wanaposhindwa kuwaridhisha wananchi kupitia utawala mbaya na ufisadi ulioota mizizi kando na matatizo mengine.

Kukwama kwao mamlakani ndiyo kiini cha wanajeshi kuingilia kuokoa raia ambao hueleza ghadhabu yao kupitia misururu ya maandamano.

Afrika ni bara ambalo japo lipo nyuma kimaendeleo ikilingalishwa na mabara mengine, halifai kutumia vita na mapinduzi kama suluhu kwa matatizo yake ya kisiasa enzi hizi.

Hata baada ya mapinduzi haya, uongozi bora unaopiganiwa mwishowe huwa haupatikani.

Baadhi ya mataifa ambayo yameshuhudia mapinduzi na kwa sasa hayako dhabiti kisiasa ni Zimbabwe na Sudan.

Mnamo Novemba 2017, utawala wa miaka 40 wa marehemu Rais Robert Mugabe nchini Zimbabwe ulifikia kikomo baada ya mkuu wa jeshi Constatino Chiwenga kuongoza mapinduzi bila umwagikaji wa damu.

Zimbabwe baadaye iliandaa kura ambapo Rais Emmerson Mnangagwa alitwaa uongozi huku Bw Chiwenga akichaguliwa makamu wa Rais.

Hadi leo, hakuna amani Zimbabwe huku maandamano yakiendelea, raia na viongozi wa upinzani wakilalamikia maisha magumu, ufisadi na kutotimizwa kwa ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi.

Kwa kifupi, raia wa Zimbabwe hawajaona tofauti zozote za uongozi wa sasa na ule wa marehemu Rais Mugabe.

Hali ni hiyo hiyo nchini Sudan Kusini ambapo hakuna utulivu wa maana tangu Rais Omar al Bashir aondolewe madarakani miaka miwili iliyopita. Serikali ya pamoja iliyoundwa na wanajeshi na wawakilishi wa raia haijawaridhisha raia hadi leo.

Hali nchini Sudan na Zimbabwe inaonyesha wazi hata mapinduzi yanaweza kuwaletea raia viongozi katili zaidi kuliko watangulizi wao.

Kisa cha Mali japo kinazua shutuma nyingi lakini pia kinaonyesha wazi kwamba viongozi wetu hawajifunzi kwa makosa yaliyotekelezwa na watangulizi wao.

Rais Ibrahim Keita alihudumu katika serikali zilizopita na hata kuwania Urais wa nchi hiyo 2002, 2007 kabla ya kushinda 2013.

Kutokana na tajriba yake ya uongozi, raia walimchagua wakiwa na matumaini kwamba angeongoza vyema na kuepuka maovu ya tawala zilizopita.

Hata hivyo, Rais Keita alifuata mkondo wa watangulizi wake huku utawala wake ukizingirwa na vita vya kikabila ambavyo vilisababisha vifo vya wengi na wengine wakalazimika kuhama makwao.

Pia, Rais Keita anadaiwa kuiba kura na kujirejesha uongozini 2018 hali ambayo iliongeza uhasama kati yake na raia.

Matukio haya yanaonyesha hata viongozi wanaofikiriwa kuwa ni malaika hubadilika na kuendeleza uongozi mbaya wanapoingia mamlakani.

Kuzuia mapinduzi ya mara kwa mara kama haya, viongozi wanafaa wajua kuwa mamlaka ni ya raia na hawawezi kuongoza milele.

Pia viongozi wetu wajizuia kuvuruga uchaguzi ili kusalia uongozini kwa kuzingatia demokrasia na kuondoka mamlakani muda wao unapotimia.

Haya mapinduzi ya kila mara yatazidi kulifanya bara hili lidharauliwe hasa na nchi za wazungu.

You can share this post!

TAHARIRI: Ufisadi hautambui mirengo ya kisiasa

MATHEKA: Serikali ilipe wahudumu wa afya kuokoa Wakenya