• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
RIZIKI: Alianza kufanya biashara baada ya kidato cha nne kutengeneza mazingira mazuri ya wadogo wake kusoma

RIZIKI: Alianza kufanya biashara baada ya kidato cha nne kutengeneza mazingira mazuri ya wadogo wake kusoma

Na FARHIYA HUSSEIN

AKITUMIA Sh75,000 alizozipata kupitia shughuli mbalimbali halali kipindi akiwa nyumbani baada ya kukamilisha elimu ya sekondari Harith Hatib Abdallah alifungua biashara yake mwenyewe badala ya kujiunga na chuo kikuu kwa masomo zaidi.

Hatib mwenye umri wa miaka 26 anasema alilazimika kufanya hivyo ili ndugu yake ajiunge na chuo kikuu.

“Mimi ni mzaliwa wa pili katika familia ya watoto watano. Tulilelewa na mama pekee na haikuwa kazi rahisi kwake kutulea sisi sote. Ilinibidi nijitoe mimi ili kufanya njia iwe rahisi kwa wadogo wangu,” Hatib anasimulia.

Anaelezea kuwa mapenzi yake ya mitindo na miundo mbalimbali ya mavazi ndizo sababu zingine za yeye kufanya biashara ya mavazi.

“Nikiwa kidato cha pili hali ilikuwa ngumu na nakiri kwamba mwaka 2014 nilianza kuuza nguo wakati shule zilikuwa zimefungwa ambapo nilikuwa nikipata Sh3,000 kila siku, ” anasema Hatib.

Haikuwa rahisi wakati alifaa kujiunga na chuo kikuu; hasa kumshawishi mama yake kwamba alit5aka sana wadogo wake wawe pahala pazuri na salama kielimu.

“Ilikuwa changamoto kumshawishi mama yangu kuwa ninataka kujiingiza kwenye biashara badala ya kujiunga na chuo kikuu,” Hatib anasema.

Mnamo mwaka wa 2016, anasema alipata msaada kutoka kwa familia; mama yake alipompa chumba kidogo na kukibadilisha kuwa duka lake ambalo kawaida hujulikana kwa jina la Last King Streetwear.

“Hapo mambo yakaanza kuboreka ambapo nilianza kupata mapato Sh20,00o kila wiki,” akasema.

Duka lake linapatikana Watamu, Kaunti ya Kilifi na hapo anauza nguo za wanawake, wanaume na watoto.

Harith Hatib Abdallah. Picha/ Farhiya Hussein

Ukifika mlangoni mwa duka hilo, ukaribishwa na michoro tofauti tofauti.

“Kama ningeenda chuo kikuu ningekuwa nikifanya kozi inayohusiana na sanaa na ubunifu. Michoro hiyo inamaanisha kuleta taswira ya tasnia ya mitindo,” anaezea akifafanua kuhusu michoro hiyo.

Anasema kuwa wateja wake wanapatikana kote nchini na wengine hufanya ununuzi kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii.

“Napeana punguzo kwa wateja wangu wakati wa likizo na wakati mwingine hutoa vifurushi vya zawadi ambavyo vina shati, suruali na jozi ya viatu,” anasema.

Mnamo Desemba 2019 Hatib anasema alibadilisha duka lake kuwa la kisasa zaidi; yaani boutique.

Huu ni mwaka wake wa saba akifanya biashara na anasema anafikiria kufungua tawi lingine hivi karibuni eneo la Malindi ambalo litaegemea zaidi katika biashara ya nguo za wanawake.

“Nyakati zingine, wateja hufanya maagizo na huwajui kamwe. Ninalazimika kutafuta suluhisho. Kila kitu kina changamoto; tunapaswa kupambana na kujipa fursa kama vijana. Wakati mwingine inakubidi ujinyime ili wengine wanufaike,” anashauri.

Ndoto yake ni kuanza kuleta nguo kutoka China na Dubai.

You can share this post!

ANA KWA ANA: Mmiliki wa Shirko Media aelezea safari yake...

BI TAIFA AGOSTI 5, 2020