• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
WASONGA: Malaria ndio ugonjwa unaoua zaidi nchini, usipuuzwe

WASONGA: Malaria ndio ugonjwa unaoua zaidi nchini, usipuuzwe

Na CHARLES WASONGA

MALARIA ni mojawapo ya magonjwa ambayo huangamiza watu wengi nchini Kenya hata kuliko maradhi mengine yasio ya kuambukiza na hata Covid-19.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Afya, ugonjwa huo huua zaidi ya watu 200 kila siku na takriban watu 22,000 kila mwaka nchini .

Ripoti kadha za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) huonyesha kuwa Kenya ni mojawapo wa mataifa ya Afrika yanayohitaji misaada kwa ajili ya kupambana na malaria.

Watoto wa chini wa umri wa miaka 5 ndio na akina mama wajawazito ndio huathirika zaidi na ugonjwa huu unaosambazwa na mbu.

Katika miaka ya nyuma, Serikali na mashirika fadhili yamekuwa yakitenga fedha nyingi za kufadhili mipango ya kuzuia, kutoa uhamasisho na kutibu malaria katika sehemu kadha nchini.

Kwa hivyo, licha ya kwamba serikali inaelekeza juhudi nyingi katika mpango wa kupambana na ugonjwa wa Covid-19, haifai kupuuza mpango wa kukabiliana na malaria.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, kaunti nyingi zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa za malaria wakati huu wa janga la corona.

Hali ni mbaya zaidi katika kaunti za Homa Bay, Siaya, Kisumu na Kericho ambako hospitali za umma hazina dawa za malaria katika vile Coartem 80/480 na Fansidar.

Uhaba huu unachangiwa na hatua ya Amerika mwaka jana kuondoa ufadhili wake wa mpango wa kupambana na malaria nchini mpango uliojulikana kama ‘President’s Emergency Plan for Aid Relief (Pepfar)’.

Mpango huo sasa unatoa fedha za ununuzi wa dawa za kukabiliana na makali ya Ukimwi, maarufu kama ARVs pekee.

Lakini wakati huu, asilimia 60 ya wagonjwa wanaofika hospitalini kusaka matibabu katika kaunti za magharibi mwa Kenya huugua malaria.

Wengi wao, haswa akina mama wajawazito, hawawezi kumudu bei ghali ya dawa za malaria ikizingatiwa kuwa kipimo (dose) moja ya dawa hizo inauzwa kwa kati ya Sh450 na Sh600.

Malaria ina hatari kubwa kwa akina mama waja wazito kwa sababu isipotibiwa katika kipindi hicho inaweza husababisha vifo.

Vile vile, husababisha hatari ya mama kujifungua kabla ya muda wake kutimu, au ajifungue mtoto mwenye uzani mdogo kupita kiasi. Watoto wanaozaliwa na mama wanaugua malaria pia hufariki mapema.

Kwa hivyo, serikali za kaunti zichukue hatua ya haraka kuzuia athari kama hizi kwa kununua dawa za malaria kwingineko wakati huu ambapo Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (KEMSA) inazongwa na sakata ya ufisadi.

You can share this post!

KAMAU: Ni wakati wa kukumbuka walimu wa chekechea

Msisimko kufuatia kutolewa ratiba ya kurejelewa michezo