Msisimko kufuatia kutolewa ratiba ya kurejelewa michezo
Na JOHN ASHIHUNDU
WADAU katika sekta ya michezo nchini hatimaye wamepata afueni baada ya serikali kutangaza muongozo wa kurejelewa kwa shughuli za spoti.
Kupitia kwa mkutano wa mtandaoni, Waziri wa Michezo, Amina Mohamed jana Jumatatu alizindua miongozo na taratibu zitakazotumiwa kurejelewa kwa michezo nchini.
Awali Amina aliteua kamati ya ushauri ikiongozwa na Waziri msaidizi Noor Hassan kushughulikia uwezekano wa wanamichezo kurejelea shughuli zao kote nchini.
Shughuli zote za michezo zilisimamishwa ghafla mwezi Machi kufuatia kuenea kwa virusi vya corona.
Lakini sasa washikadau wamepewa siku saba kusoma nakala ya kurasa 16 na kupeana mapendeezo yao, kabla ya wizara kuamua tarehe kamili ya kurejelewa kwa shughuli hizo.
“Kufuatia hali tata ya janga la corona, ilibidi Wizara ya Afya Shirikisho la Afya Ulimwenguni (WHO) ichukue tahadhari zifaazo kwa kujumuisha umma. Natarajia majibu haraka iwezekanavyo ili turejelee shughuli zetu za michezo,” alisema Waziri Amina huku akieleza matumaini yake makubwa ya shughuli hizo kurejelewa haraka iwezekanavyo kote nchini.
“Ningependa kuwapongeza wanakamati walioteuliwa kwa kufanya kazi yao kwa bidii kuhakikisha kila kitu kinafanywa kitaalamu. Tumepoteza muda mrefu mwaka huu na jinsi mjuavyo, shule zilifungwa ghafla na wanafunzi wamepoteza wakati wao mwingi, na hatutaki hali kama hiyo ikivuruga sekta ya michezo. Tunataka kurejelea shughuli zetu za michezo kote nchini,” alisema Hassan ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo.
Kulingana na miongozo iliyowekwa, mashirika yote ya michezo lazima yahakikishe taratibu za kukabili Covid-19 yanazingatiwa na wanamichezo, wakufunzi wao pamoja na watu wengine wa kujitolea. Viwanja vyote vitakavyotumika sharti vipuliziwe dawa ya kuzima viini vya corona na magonjwa mengine yoyote ya kuambukiza.
Maafisa wote, wanahabari na wafanyakazi katika viwanja mbali mbali vya kuchezewa lazima wafanyiwe vipimo vya Covid-19 mara kwa mara.
Mahojiano yote yatafanyika pasipo kutangamana (umbali wa mita 1.5 au zaidi). Wachezaji na wahusika wengine hawatakubaliwa kuamkuana wakati wa michezo, na pia wachezaj hawatakubaliwa kubadilishana nguo.
Timu zitatakiwa kuwa katika sehemu moja hadi mwisho wa mechi. Washirikishi watatakiwa kuweka rekodi za wachezaji wote ili wapatikane kila wanapohitajika.
Kisa chochote cha Covid-19 kitatatuliwa kulingana na miongozo ya Waziri wa Afya.
Kutakuwa na watu maalum katika kila mlango wa kuingia uwanjani kwa lengo la kujulisha umma kuhusu taratibu za kuepuka maambukizi ya Covid-19 na pia kupima halijoto.
Mtu yeyote atakayepatikana na kiwango cha halijoto kinachozidi nyuzi 37.5 hatakubaliwa kuingia uwanjani.