ODONGO: Kauli ya Raila kuidhinisha Nyong'o ugavana haifai
Na CECIL ODONGO
JAPO chama cha ODM kimekuwa kikijivumisha kama kinachozingatia demokrasia, kauli ya kinara wake Raila Odinga kuhusu uwaniaji wa ugavana wa Kaunti ya Kisumu mnamo 2022 ilidhihirisha kinyume.
Bw Odinga wiki jana akiwa katika kaunti hiyo alimwidhinisha Gavana Profesa Anyang’ Nyong’o kuhifadhi kiti chake kwa kipindi cha pili, akimsifu kwa utendakazi wa kuridhisha na kung’arisha mji wa Kisumu.
Kauli hii ya Bw Odinga haikufaa kwa kuwa amekuwa akisema kila mara kwenye mikutano au vikao na vyombo vya habari kwamba ni mapema sana kuanzisha kampeni za 2022.
Je, ni sawa kuidhinisha wawaniaji wa ugavana jinsi alivyofanya kwa Profesa Nyong’o na wakati huo huo kukemea mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto kwa kufanya kampeni?
Pili, kumpendelea Profesa Nyong’o kunawanyima baadhi ya viongozi ambao wangependa kupigania tiketi ya ODM kwenye mchujo kushiriki shughuli hiyo.
Baadhi ya wanaomezea mate tiketi ya ODM katika kaunti hiyo ni Seneta wa Kisumu Fred Outa na aliyekuwa Gavana Jack Ranguma miongoni mwa wawaniaji wengine wengi.
Kuwanyima wawaniaji hawa nafasi ya kugombea tiketi ya chama huenda kukaikosesha ODM kiti hicho iwapo waliozuiwa ni maarufu miongoni mwa raia.
Kwenye uchaguzi wa 2013, chama hicho kilipoteza kiti cha ugavana wa Migori mwaniaji wake Akong’o Oyugi alipobwagwa vibaya na Gavana Okoth Obado ambaye alichezewa shere kwenye mchujo na akahamia People Democratic Party (PDP).
Kudhihirisha umaarufu wake, Bw Obado alirejea ODM mnamo 2017 na kumbwaga Ochillo Ayacko kwenye mchujo na hata uchaguzi mkuu. Bw Ayacko hata hivyo, alichaguliwa Seneta kwenye uchaguzi mdogo baada ya mauti ya marehemu Ben Oluoch Okello 2018.
Japo huenda Profesa Nyong’o amefanya kazi nzuri kimaendeleo hasa kurembesha jiji la Kisumu, hapakosi wakazi hasa maeneo ya mashinani ambao hawajaona matunda ya utawala wake.
Kumpokeza tiketi ya chama huenda kukawafanya wasioridhishwa na utawala wake kuwapigia wawaniaji wa vyama vingine au wagombeaji huru na kudidimiza matumaini ya chama kukinyakua kiti hicho muhimu kwenye ngome yake.
Ni wiki jana tu ambapo Bw Odinga alizindua bodi ya uchaguzi wa ODM ambapo yeye na waliohutubu waliahidi kwamba mchujo wa chama utakuwa huru na haki.
Kama kiongozi ambaye tamko lake kuhusu uchaguzi huwa halipingwi na wakazi wa Nyanza, kumwidhinisha Profesa Nyong’o ni kama kumhakikishia tayari ameshinda kiti hicho na bodi haitakuwa na haja ya kusimamia mchujo wa ugavana Kisumu.
Je, huu mtindo wa kuwaidhinisha wawaniaji wa ODM ukiendelea maeneo mengine basi kazi ya uchaguzi itakuwa nini?
Iwapo ODM itaendelea kuwafumba wafuasi wake macho kwa kuunda bodi ya uchaguzi ilhali kwa upande mwingine viongozi wasio imara wanaidhinishwa, basi viti vinavyoshikiliwa na chama vitaendelea kupungua kila uchaguzi.
Kisumu ndio kaunti ya Luo Nyanza ambayo Gavana wake atatetea wadhifa wake huku Cornel Rasanga (Siaya), Okoth Obado (Migori) na Cyprian Awiti (Homa Bay) wakimaliza mihula yao miwili.
Wakazi wake wanafaa wapewe nafasi ya kutathmini utendakazi wa Profesa Nyong’o na kujiamulia wenyewe badala ya kushawishiwa kumuunga mkono.
Kaunti ya Kisumu haihitaji kiongozi ambaye lengo lake kuu ni kuonyesha utiifu kwa chama pekee bali yule wa kupambana na matatizo kama janga la mafuriko, kuporomoka kwa viwanda vya sukari na matatizo ya wakulima wa mpunga kati ya mengine mengi.