NGILA: Baada ya kujenga vituo nchini, tugeuze data iwe dijitali
Na FAUSTINE NGILA
JUZI nilizuru kituo kipya cha data kinachojengwa katika eneo la Milimani, Nairobi ambapo mamilioni yamewekezwa katika hifadhi ya data.
Ni kituo cha tatu sasa nchini Kenya, hali inayoashiria mageuzi yanayotarajiwa katika ulingo wa teknolojia miaka michache ijayo.
Wataalamu wamesisitiza kuwa matumizi ya data ndiyo huduma ambayo itakuwa na thamani ya juu zaidi ulimwenguni, na kampuni kadha zimejizatiti kujenga vituo vya kuhifadhi data kwa mamia ya kampuni na mashirika barani Afrika.
Ingawa utafiti wa sasa unaonyesha kuwa Afrika ndilo bara lililosalia na fursa za kukuza biashara kupitia teknolojia, tayari dunia inasonga kwa mwendo wa kasi mno, hivi kwamba bara hili limesalia nyuma kiteknolojia.
Humu nchini kwa mfano, tunaposema kuwa tuko tayari kuwekeza kwa vituo vya data, twajihadaaa wenyewe maanake data nyingi katika mashirika ya serikali na kampuni za kibinafsi bado imehifadhiwa katika miundo ya kikale.
Data kuhusu wagonjwa katika Hospitali Kuu ya Kenyatta bado imenakiliwa katika karatasi na vitabu. Ukienda pale utaona rundo la majitabu katika kila idara.
Katika mashirika mengine ya kiserikali kama Kenya Airways, Mamlaka ya Bandari, Bodi ya Utalii ya Kenya, Idara ya Mahakama, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, Idara ya Polisi, Kenya Power, Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya, vyuo vikuu na shule, bado data inazidi kuhifadhiwa katika miundo ya zamani isiyoweza kugeuzwa kuwa suluhu kwa wananchi.
Ingawa Kenya imejizolea sifa za kuwa mstari wa mbele katika matumizi ya teknolojia, ukosefu wa data ya kidijitali unaendelea kuhujumu juhudi zote za ubunifu wa kisasa unaotegemea data kufanya maamuzi.
Hivyo, ni wazo zuri kwa wawekezaji kujenga vituo vya data nchini ila kufanikisha malengo yao ya kugeuza mashirika haya kuwa wateja, kunafaa kuanza kwa kuyarai yageuze data yao iwe ya kidijitali. Huwezi kuhifadhi karatasi au vitabu vya taarifa kwenye seva za Intaneti.
Jinsi vituo hivi vya data vinavyojengwa pia kunaashiria mapungufu makuu katika uwezo wa Afrika wa kutumia data ipasavyo.
Kampuni za mataifa yaliyoendelea kama Google na Microsoft, kwa mfano, hazijengi vituo vyake katika orofa za majengo marefu kama inavyofanyika hapa Afrika. Kutokana na joto jingi linalotokana na usasisho wa data kwa seva, kibaridi huhitajika kupunguza joto hilo.
Hapa Kenya, wahandisi wanatumia nyaya za hewa baridi kupunguza joto hilo lakini Microsoft sasa imeweka seva zake ndani ya bahari ili pia kuzuia uwezekano wa moto kutokea na kuwezesha matumizi ya kawi safi. Nazo seva za Google zinaelea baharini.
Kifupi, tunapofikiria kuwekeza katika jambo lolote, tunafaa kuzingatia mustakabali wa mradi huo kwa kutafiti kuhusu mageuzi ya kisasa.
Ila ni hatua ya maana kwa Kenya kuzipiku nchini zingine barani katika uhifadhi wa data, tunafaa kuhakikisha vituo hivi vitakuwa na watumizi, kwa kuanza kuwekeza katika kuongeza kiwango cha data ya kidijitali nchini.
Tusisahau kuwa uvumbuzi wowote wa kisasa unatumia data ya kidijitali, na kukabiliana na changamoto zilizopo hapa barani, basi tunafaa kuanzia panapostahili. Tukome kutegemea data ya kikale.