• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
KINA CHA FIKIRA: Shida huzunguka, leo kwangu kesho yaweza kuja kwako

KINA CHA FIKIRA: Shida huzunguka, leo kwangu kesho yaweza kuja kwako

Na WALLAH BIN WALLAH

DUNIA ni duara.

Na maisha ni mabadiliko. Leo hivi, kesho vile! Kuna kupata na kukosa. Ukibahatika kupata umshukuru Mungu, wala usimcheke mtu ambaye hajapata! Heri kuhurumiana na kusaidiana tu. Unayemsaidia leo huenda akakusaidia kesho! Shida huzunguka. Leo kwangu kesho kwako!

Bwana Kiki alikuwa na hoteli iliyopendwa sana katika mji mdogo wa Kazimali. Watu wengi walikula hapo hasa siku za soko! Walipata vyakula vya aina nyingi na kunywa supu tamu. Walipokuwa wakiendelea kula saa saba na nusu hivi, mgeni aliyevaa magunia machafu yaliyoraruka alifika pale na kusimama karibu na pipa la kutupia takataka na mabaki ya vyakula. Huyo alikuwa masikini mwendawazimu aliyeitwa Jenerali. Kila mtu alimjua pale mjini Kazimali kwa upole wake na alivyoomba pesa au chakula kwa heshima!

Subira, msichana mfanyakazi wa hoteli, alipomwona akamuuliza kwa upole, “Jenerali, unasemaje?”

Jenerali alijibu polepole, “Nina njaa! Naomba kuchukua chakula cha ndani ya pipa nile!”

Subira alienda kumwombea idhini kwa mwenye hoteli.

Bwana Kiki alipoambiwa alitoka nje kwa kelele, “Yuko wapi huyo mwendawazimu? Sitaki uchafu hotelini kwangu!”

Akachukua ndoo iliyojaa maji machafu akammwagia Jenerali akisema, “Ondoka kabla sijakumwagia maji moto!”

Watu waliokuwa wakila walishangaa! Wengine wakasema, “Apewe chakula, tutamlipia!” Lakini Kiki mwenye hoteli alikataa katakata! Akamfukuza Jenerali kwa ukali! Jenerali alienda na njaa yake huku mwili umelowa maji! Subira na watu wengine walisikitika sana!

Wiki mbili baadaye, Bwana Kiki aliondoka saa nne asubuhi amevalia suti nzuri akipitia kichochoroni kuelekea katikati ya mji akiwa amebeba mfuko mkubwa mkononi.

Vijana watatu wenye visu walitokea ghafla wakamvamia na kumwangusha chini! Wakamnyang’anya mfuko na simu zake mbili, wakakimbia! Punde, mtu wa ajabu alitokeza mbio kichakani akamfuata kijana aliyetoroka na mfuko. Baada ya kupiga kona sita, mtu huyo alimtega kijana akaanguka na mfuko ukadondoka! Mtu huyo aliuokota mfuko kumpelekea Kiki aliyekuwa akilia, “Pesa zangu shilingi laki mbili (200,000) nilizokuwa nikipeleka benkini! Uuuwi!!”

Bwana Kiki alipomwona mtu mchafu aliyevaa magunia akimpa mfuko wake wa pesa, alishtuka akasema, “Jenerali! Ni wewe!!?” Jenerali akajibu, “Ni mimi Jenerali! Chukua pesa zako na kitambulisho chako pamoja na kitabu cha hundi au cheki, Bwana Kiki mwenye Hoteli Suputamu!” Kiki alimkumbatia Jenerali akilia kwa uchungu! Akamshika Jenerali mkono kurudi naye hotelini!

Ndugu wapenzi! Dunia duara! Maisha ni mabadiliko! Huwezi kujua atakayekusaidia kesho! Tuhurumiane na kusaidiana! Kila mtu ni mtoto wa Mungu! Shida haina mwenyewe! Leo kwangu kesho kwako! Tusaidiane tu!

You can share this post!

NGILA: Baada ya kujenga vituo nchini, tugeuze data iwe...

GWIJI WA WIKI: Shullam Nzioka