Michezo

Golikipa Oyemba wa Harambee Stars sasa andazi moto kwa vikosi saba ndani na nje ya nchi

August 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

LICHA ya kutoshiriki mchuano wowote tangu Novemba 2019 golikipa matata wa Harambee Stars, John Oyemba, amethibitisha kwamba huduma zake zinawaniwa na vikosi saba tofauti ndani na nje ya nchi.

Mlinda-lango huyo alipata jeraha baya la mgongo mwaka 2019 na akasalia bila klabu mnamo Januari 2020 baada ya mkataba wake na Kariobangi Sharks kutamatika rasmi.

Hata hivyo, wingu la matumaini limeanza kumshukia mwanafunzi huyo wa zamani wa Shule ya Upili ya Jamhuri ambaye kwa sasa anafukiziwa na klabu tano za humu nchini na mbili za ughaibuni.

Tusker, AFC Leopards, Posta Rangers, Nairobi City Stars na Bidco United ni miongoni mwa vikosi vya Ligi Kuu ya Kenya ambavyo vimeanika maazimio ya kujitwalia huduma za Oyemba.

Nyota huyo hata hivyo amekataa kufichua majina ya klabu za nje zinazohemea maarifa yake japo amedokeza kwamba ni za Afrika Mashariki.

Ingawa Gor Mahia walikuwa pia wakizikeshea huduma zake, mabingwa hao mara 19 wa KPL walijiondoa kwenye vita vya kumsajili Oyemba na badala yake wakamwendea aliyekuwa kipa wa City Stars, Levis Opiyo.

Oyemba, ambaye alikuwa akishiriki mazoezo ya pamoja na wanasoka wa Tusker kabla ya kampeni za msimu huu wa 2019-20 kutamatishwa ghafla mnamo Aprili, amesema kwamba amepona kabisa na ana kiu ya kurejea uwanjani kwa minajili ya msimu mpya.

“Nina ofa saba ninazozitathmini kwa pamoja na wakala wangu. Najihisi vizuri kwa sasa na daktari amenikubalia kuanza kushiriki mazoezi mazito. Natazamia kupata mwajiri mpya hivi karibuni na kujivunia msimu wa kuridhisha,” akasema Oyemba.

Kwingineko, Wazito FC waliendelea kujishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho wa wachezaji baada ya kuthibitisha kumsajili kiungo mkabaji Castro Ogendo kutoka Gor Mahia.

Ogendo ambaye ni sajili wa tisa wa Wazito FC muhula huu, atalazimika kupigania nafasi katika kikosi cha kwanza na Anthony Njeru, Jackson Juma na David Oswe.

Mwanafunzi huyo wa zamani wa Ambira High, amewahi pia kuvalia jezi za Bidco United katika Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).