AWINO: Ushuru kwa mazao ya kilimo wafaa kushughulikiwa upya
Na AG AWINO
KATIKA kipindi kilichopita, Waziri wa Kilimo Peter Munya aliorodhesha mimea ya mahindi, miwa, chai, pareto na kahawa katika kiwango sawa.
Hii ni kumaanisha ya kwamba sheria zinazoongoza mimea hii zitakuwa sawa bila kuzingatia aina ya mmea.
Hapo awali, mimea kama miwa ilikuwa ikiongozwa na mfumo tofauti wa sheria. Hii ni habari njema kwani sheria husaidia katika kusawazisha mazingira ya kilimo nchini.
Aidha, aliwasilisha mapendekezo mapya ya sheria kuhusu majanichai kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla kuziweka rasmi kwenye Gazeti la Serikali.
Hata hivyo, zipo changamoto na ukosefu wa usawa katika kilimo ambazo zinafaa kumulikwa. Kwa mfano, katika sekta ya miwa, wakulima wamekuwa wakilalamimika kuondolewa kwa ushuru wa maendeleo, almaarufu (SDL) katika miaka iliyopita.
Kilio hiki kilisikika na hatimaye ushuru huo kurudishwa kama ilivyokuwa zamani. Kodi hiyo asilimia nne ya mauzo ya sukari.
Hii ni habari njema kwa sekta ya sukari kwani ushuru huu umekuwa ukitumiwa katika kugharimia maendeleo kama vile ujenzi wa miundomsingi, kutoa mikopo ya maendeleo nyanjani ambapo wakulima na kampuni za sukari zipo. Wakati ushuru wa SDL ulikuwa hautozwi, kiwango cha maendeleo kilishuka chini mno.
Kinaya cha kulilia ushuru kutozwa huku wenzao wa majani chai wakilalamikia adhabu ya ushuru kwao.
Ushuru unaotozwa kwa kampuni zote 54 ni aina 42 tofauti. Kabla wakulima kulipwa marupurupu yao ya kila mwaka, sharti watozwe pesa nyingi.
Malipo haya hutozwa na, kwa mfano, Halmashauri ya Ushuru Nchini (KRA), Halmashauri ya Kilimo na Vyakula (AFA), Halmashauri ya Ubora wa Bidhaa (KEBS), NEMA, KEPHIS, Kaunti, Halmashauri ya Bandari Nchini (KPA) na asasi nyingine thelathini na sita.
Hali hii imechangia kudorora kwa hali ya kiuchumi ya wakulima wengi wa majanichai nchini. Imekuwaje mfumo wa ushuru kwa mmea mmoja ni tofauti na mfumo mwingine kama vile miwa?
Hivi majuzi, Waziri wa Fedha Ukur Yatani alitoa onyo kwamba KRA mwaka huu itakusanya asilimia 30 tu ya ushuru. Hii nikumaanisha ya kwamba KRA itakosa kutimiza malengo yake kifedha ya mwaka wa 2020 kwa asilimia 70.
Kwa maoni yangu, hamu na ari ya kukusanya kiwango cha juu cha ushuru ndiyo ambayo inachangia kutozwa kwa ushuru kuumiza wakulima wa majanichai.
Baraza la Magavana na wanasiasa wanaotoka katika sehemu za kukuza majanichai hawajakemea hali hii ambayo inazidi kudhulumu wakulima wa majanichai.
Sijamsikia Katibu Mkuu wa Wafanyakazi Francis Atwoli akikemea dhuliuma hii. Ni ushuru wa majanichai ambao utawezesha Serikali kutimiza malengo yake ya kifedha? Si haki kuendelea kutoza sehemu moja ya kilimo na kudekeza sehemu nyingine.
Hoja kuhusu ushuru na kutoza kwa njia isiyofaa imekuwepo tangu ripoti kuhusu ushuru iliyotolewa na shirika moja la kimataifa kuorodhesha Kenya kama nchi ambayo ina mfumo mkali sana kiushuru na kinachopita kiwango kinachokubalika duniani kwa asilimia 43.1
Na Licha ya kwamba mashirika mbalimbali nchini Kenya hulipa aina za ushuru 41 tofauti, wakulima wa sekta ya majanichai bado wako juu kwa kulipa aina 42 za ushuru. Kwa kawaida, mashirika mengine katika nchi nyingine duniani hulipa aina 27 ya ushuru kwa serikali zao.
Wakati umewadia wa kusawazisha ushuru kuhusu kilimo au kuangalia upya mfumo wa ushuru unaotozwa wakulima wa majanichai ili kuimarisha hali yao kiuchumi nchini, kwani hakuna nchi iliyowahi kutajirika kutokana na ushuru mwingi.
AG Awino ni mwanamawasiliano anayefuatilia kwa makini kilimo nchini.