Siasa

Kauli ya Rais kuhusu Katiba yaibua mjadala

August 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

KAULI ya Rais Uhuru Kenyatta kwamba ni lazima katiba ya Kenya iliyopitishwa miaka 10 iliyopita ifanyiwe mageuzi, imezua mdahalo mkali kati ya wanasiasa wanaounga handisheki, wanaharakati na wataalamu wa masuala ya kikatiba.

Huku wanasiasa wanaounga serikali wakiunga kauli hiyo, wanaharakati na wataalamu wa masuala ya katiba wanasema haifai kubadilishwa kabla ya kutekelezwa kikamilifu.

Kulingana na mtaalamu wa masuala ya kiuchumi, Bw David Ndii, Katiba ya Kenya inahitaji kutekelezwa na sio kubadilishwa.

Bw Ndii anasema Rais Uhuru Kenyatta haipendi katiba ilivyo kwa wakati huu na ndio sababu anataka ifanyiwe mageuzi.

“Katiba ya Kenya ya 2010 imenusurika kwa miaka 10 licha ya Uhuru Kenyatta kuishambulia na kuikaidi kwa kila namna. Katiba yetu wakati wa uhuru haikuwa na bahati. Katiba ya Kenya ya 2010 ni nzuri, imetulinda kutoka hujuma za serikali,” Bw Ndii alisema.

Aliyekuwa Jaji MKuu Dkt Willy Mutunga alisema kwamba wanasiasa hawawezi kuimarisha katiba ambayo hawajaonyesha kujitolea kutekeleza.

Akihutubia taifa Jumatano; mkesha wa maadhimisho ya miaka kumi tangu katiba mpya ilipozinduliwa, Rais Kenyatta alisema wakati umefika wa kurekebisha katiba ili kuifanya bora zaidi. Rais alisema marekebisho hayo yatakayofanywa kupitia Mpango wa Upatanishi (BBI) utaunganisha Wakenya.

Hata hivyo, Dkt Mutunga anasema wanasiasa hawawezi kutegemewa kuleta mageuzi ya kikatiba ambayo wamekuwa wakikaidi. Rais Kenyatta na maafisa wa serikali wamelaumiwa kwa kupuuza utawala wa sheria.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chama Cha Wanasheria Kenya (LSK) Nelson Havi, viongozi wa sasa hawawezi kutegemewa kwa mageuzi ya kikatiba yanayofaidi mwananchi wa kawaida kwa kuwa hawajaitekeleza kikamilifu.

Mtetezi wa haki za binadamu John Githongo na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kutetea haki la Transparency International Sheila Masinde wanasema kwamba katiba hufanyiwa mageuzi baada ya kutekelezwa kikamilifu na uchunguzi kufanywa kubaini mapungufu yake.

“Ni viongozi wa kisiasa ambao wamekosa kufanyia haki katiba ambayo imetajwa kuwa mojawapo wa zile bora duniani. Wanahitaji kuitekeleza ilivyonuiwa ili kila Mkenya afurahie manufaa yake badala ya kuifanyia mageuzi,” akasema Bw Githongo.

Kulingana na Bi Masinde, katiba inaweza kurekebishwa tu iwapo uwezo wake umepimwa baada ya kutekelezwa kikamilifu. Naye Profesa Yash Pal Ghai ambaye aliongoza mchakato wa kuandika katiba mpya anaonya Wakenya dhidi ya kukaribisha mageuzi ya kikatiba.

“Hatufai kufurahia na kusherehekea maadhimisho ya miaka kumi ya katiba. Hatuna sababu ya kuamini kwamba itatupatia matokeo bora kuliko miaka kumi iliyopita ikizingatiwa mikono ambayo imeangukia,” akasema Profesa Ghai.

Mojawapo ya marekebisho ambayo wanasiasa wanataka ni mfumo wa uongozi utakaobuni nafasi za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili. Kulingana na Profesa PLO Lumumba ambaye alichangia kubuniwa kwa katiba mpya, shida ya Kenya sio mfumo wa uongozi mbali ni kuingizwa kwa ukabila katika siasa.

“Shida yetu ni utamaduni wa siasa zetu, sio mfumo wa urais au wa ubunge. Nani alisema waziri mkuu ataleta tofauti yoyote? Shida yetu ni siasa zetu zinazoongozwa na ukabila,” akasema Profesa Lumumba.

Mhadhiri wa chuo kikuu cha Nairobi Dkt Wandia Njoya na kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua wanasema kwamba nia ya wanasiasa kurekebisha Katiba ni kupokonya raia nguvu wanazopatiwa na Katiba ya 2010.

“Katiba inapatia raia nguvu lakini wanaotaka irekebishwe wanataka kutwaa nguvu hizo,” Bi Karua alisema.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen alisema kwamba marekebisho ya kikatiba yanalenga kurejesha mamlaka ambayo rais alipokonywa na katiba mpya.