• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Chelsea wamsajili beki Thiago Silva kutoka PSG

Chelsea wamsajili beki Thiago Silva kutoka PSG

Na CHRIS ADUNGO

BEKI matata mzawa wa Brazil, Thiago Silva, amejiunga rasmi na Chelsea ya Uingereza kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 atakuwa na fursa ya kurefusha muda wake uwanjani Stamford Bridge kwa mwaka mmoja zaidi kutegemea matokeo yake msimu ujao wa 2019-20.

Silva alitua Chelsea bila ada yoyote baada ya mkataba wake na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu. Sogora huyo alikuwa sehemu ya kikosi cha PSG kilichopokezwa kichapo cha 1-0 na Bayern Munich ya Ujerumani katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti 23, 2020.

Kocha Frank Lampard amesema kwamba ujio wa Silva kambini mwake utaimarisha zaidi safu ya ulinzi ya kikosi hicho kilichofungwa idadi kubwa zaidi ya mabao (54) miongoni mwa vikosi vilivyokamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika nafasi ya 10-bora mnamo 2019-20.

“Nafurahia sana kujiunga na Chelsea. Ni fahari tele kuwa sehemu ya kikosi kinachonolewa na Lampard. Niko hapa kushinda mataji ya EPL kutambisha Chelsea katika soka ya bara Ulaya,” akasema Silva.

Nyota huyo ambaye amewajibishwa na timu ya taifa ya Brazil mara 88, anajivunia kuvalia jezi za PSG zaidi ya mara 200 katika kipindi cha miaka minane iliyopita ambayo imemshuhudia akinyanyua mataji saba mfululizo ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue1).

Silva ni mwanasoka wa tano kusajiliwa na Chelsea muhula huu baada ya beki Malng Sarr aliyeagana na Nice, beki wa kushoto Ben Chilwell aliyebanduka Leicester City, fowadi Hakim Ziyech aliyetokea Ajax na mshambuliaji Timo Werner ambaye alikatiza uhusiano wake na RB Leipzig.

Chelsea ambao watafungua msimu mpya wa EPL dhidi ya Brighton mnamo Septemba 14, 2020 uwanjani American Express, wanahusishwa pia na uwezekano mkubwa wa kumsajili mvamizi Kai Havertz, 21, kutoka Bayer Leverkusen nchini Ujerumani.

You can share this post!

MWANGI: Vijana wasisingizie ukosefu wa kazi nchini kuwa...

‘Tangatanga’ wawekea DCI na EACC presha