Habari

Visa vya utapiamlo vyaongezeka Mombasa

August 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MISHI GONGO

MAAFISA na wataalamu wa afya katika Kaunti ya Mombasa wameelezea hali ya wasiwasi kufuatia kukithiri kwa visa vya utapiamlo miongoni mwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano tangu kuzuka kwa janga la corona.

Utapiamlo ni ugonjwa wa mtu kukosa kupata viiinilishe muhimu katika chakula.

Akiongea na Taifa Leo Mratibu wa kushuhulikia lishe bora katika kaunti hiyo Bi Esha Bakari alisema Ijumaa hali hiyo inatokana na ugumu wa maisha ambao umewafanya wazazi wengi kushindwa kuwapa watoto wao lishe bora.

Aidha alisema janga hilo pia limetatiza kupeanwa kwa virutubisho vya Vitamini A vinavyotolewa hospitalini kwa watoto.

Alisema Vitamini A hutolewa kati ya mwezi Mei na Oktoba lakini kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19, walilazimika kusitisha chanjo hiyo.

“Janga la corona limeathiri pakubwa hali ya kifedha miongoni mwa wakazi wengi, hivyo wazazi wanashindwa kuwapa watoto wao lishe bora; hali inayowafanya kupata utapiamlo,” akasema Bi Bakari.

Bi Bakari alisema kutatua hali hiyo, Kaunti ya Mombasa imeshirikiana na shirika la hazina ya watoto ya umoja wa kimataifa (Unicef) kuwapa kina mama wenye watoto wadogo mikanda itakayowasaidia kufuatilia kukua kwa watoto wao.

Mkanda huo unasaidia kina mama kupima sehemu ya juu ya mkono wa mtoto ili kugundua ishara za utapiamlo.

Alisema mwezi Juni kupitia ufadhili wa Unicef kanda 79,999 ziligawanywa katika maeneobunge yote ya Mombasa.

“Kaunti hii ilipima watoto 104,919 katika shughuli hiyo ambayo lilifanyika kwa wiki moja. Kati ya idadi hiyo watoto 335 walipatikana kuwa na kiwango cha chini cha utapiamlo huku watoto 91 wakiwa katika hali mbaya,” akasema Bi Bakari.

Alieleza kuwa katika eneobunge la Changamwe watoto 35,466 walipimwa, 70 kati yao walipatikana kuwa na viwango vya chini vya utapiamlo huku 17 wakiwa na viwango vya juu.

Eneobunge la Kisauni kati ya watoto 24,989 waliopimwa 93 walikuwa na viwango vya chini vya utapiamlo huku 19 wakiwa hali mbaya.

Likoni ndiyo iliyoongoza kwa kuwa na visa vya juu zaidi vya watoto wanaougua utapiamlo. Kati ya watoto 29,995 waliopimwa 94 walipatikana wakiwa na viwango vya chini vya utapiamlo huku 41 wakiwa hali mbaya.

Eneobunge la Mita walipatikana watoto 78 waliokuwa na viwango vya chini vya ugonjwa huo huku 14 wakiwa hali mbaya kutoka kwa jumla ya watoto 14,470 waliopimwa.

“Janga la corona lilipozuka tulilazimika kusitisha mambo mengi kama njia ya kuwakinga watoto wadogo. Hata hivyo katika Kaunti ya Mombasa tumeanza shughuli ya kupeana Vitamini A kwa ushirikiano na maafisa wa afya ambao tumewahimiza wazingatie masharti yote ya kujikinga wasipate ugonjwa wa Covid-19,” akasema.

Alisema kufikia sasa wamepeana Vitamini A kwa watoto 183,982 mjini humo licha ya changamoto za ugonjwa huo hatari.