• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:10 PM
JAMVI: Uhuru anatumia mbinu za Moi kuwaacha wanasiasa upwekeni

JAMVI: Uhuru anatumia mbinu za Moi kuwaacha wanasiasa upwekeni

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta amefanikiwa kuwatenganisha viongozi wakuu wa kisiasa na kuwaacha wakiwa wapweke.

Rais Kenyatta amefaulu kupasua muungano wa NASA na kuvuruga vyama vya Jubilee, Amani National Congress (ANC), Wiper na Ford-Kenya.

Wadadisi wa kisiasa wanasema kuwa Rais Kenyatta anatumia mbinu za mkufunzi wake wa kisiasa Rais Mstaafu hayati Daniel arap Moi aliyekuwa mweledi wa kugawanya na kuwatenga wanasiasa kwa lengo la kuwamaliza kisiasa.

Nyadhifa muhimu

Baada ya wandani wake kupokonywa nyadhifa muhimu katika Bunge la Kitaifa na Seneti, Naibu wa Rais William Ruto sasa anaonekana mpweke.

Wandani wa Ruto waliosalia wameshikilia nyadhifa muhimu ndani ya chama cha Jubilee wametimuliwa huku wengine wakisalia afisini bila mamlaka yoyote.

Miongoni mwa maafisa wa Jubilee waliojipata taabani ni Bw Joseph Mulili ambaye amekuwa mwandani wa Dkt Ruto kwa muda mrefu tangu enzi za chama cha kilichovunjiliwa mbali cha URP.

Bw Mulili alitimuliwa kwa madai ya kutoa taarifa za siri kwa Dkt Ruto.

Japo mkurugenzi wa usajili wa wanachama wa Jubilee Bw Nick Bore anaendelea kuhudumu, amepunguziwa mamlaka na afisi yake imesalia bila kazi.

Bw Bore amezuliwa kufikia sajili wa wananchama ambazo zimehifadhiwa katika afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Dkt Ruto tayari ameelezea azma yake ya kuunda chama mbadala atakachotumia kuwania urais 2022 huku akisema kuwa Jubilee imenyakuliwa na ‘mafisi’pamoja na walaghai.

Lakini wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Naibu wa Rais Ruto ambaye amegeuka kuwa mkosoaji mkuu wa serikali ya Rais Kenyatta, hafai kujiuzulu wakati huu.

“Ruto akijiuzulu wakati huu atapoteza umaarufu na ushawishi wa kisiasa na pia atatoa mwanya wa kuhangaishwa na serikali kwa lengo la kumlemaza kisiasa. Naibu wa Rais aendelee kuwa afisini licha ya kukosa ushawishi serikalini,” anasema Profesa Medo Misama.

“Ikiwa Dkt Ruto anataka kujiuzulu angojee hadi mwanzoni mwa 2022 na kisha azindue chama kipya,” anaongezea.

Duru za kuaminika pia zinasema kuwa wakuu serikalini wamezima juhudi za mrengo wa Dkt Ruto kutaka kusajili chama kwa jina la Jubilee Asili.

Prof Macharia Munene anasema kuwa Naibu wa Rais Ruto atakuwa mpweke zaidi iwapo atathubutu kupinga kura ya maamuzi kufanyia mabadiliko Katiba.

Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wamekuwa wakisisitiza kuwa ni sharti Katiba ifanyiwe mabadiliko kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 kwa kuzingatia mapendekezo ya jopokazi la Mpango wa Maridhiano (BBI).

“Jinsi mambo yalivyo kwa sasa kuna uwezekano kwamba Naibu wa Rais atapinga kura ya maamuzi. Upande wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ukishinda, Dkt Ruto atakuwa amelemazwa kisiasa na wandani wake watamtoroka,” anasema Prof Macharia.

Dkt Ruto amenukuliwa mara kadhaa akisema kuwa hataki kuendesha kampeni mara mbili; wakati wa kura za maamuzi na Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Uchaguzi Mkuu

Japo Bw Odinga kwa sasa anaonekana kuwa na ushawishi serikalini, wadadisi wa kisiasa wanaonya kuwa atajipata mpweke iwapo atatelekezwa na Rais Kenyatta kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Ikiwa Rais Kenyatta na Bw Odinga watakosana kabla ya 2022, wadadisi wanasema, kiongozi wa ODM atajipata mpweke kwani tayari amtenganishwa na viongozi wengine wa NASA ambao wanamuona kama msaliti.

“Bw Odinga amekuwa akifanya kila kitu kuhakikisha kuwa uhusiano wake wa na Rais Kenyatta hautasambaratika.

“Tumeona chama cha ODM kikijitokeza kutetea serikali kuhusiana na sakata ambapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya vita dhidi ya virusi vya corona zinadaiwa kuibwa. Hizo zote ni juhudi za Bw Odinga kuonekana mwaminifu kwa Rais Kenyatta,” anasema Prof Misama.

Anasema kuwa huenda kuna mkono wa serikali katika masaibu yanayomkumba kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi.

Juhudi za Mudavadi kutaka kubadilisha katiba ya chama ili kumwezesha kuendelea kuwa kiongozi wa ANC kwa miaka mitano zaidi, ziligonga mwamba wiki iliyopita baada ya msajili wa vyama vya kisiasa kukataa mabadiliko hayo.

Msajili wa vyama Ann Nderitu alikataa ombi hilo akisema kuwa Bw Mudavadi hakufuata katiba ya ANC na Sheria ya Vyama vya Kisiasa.

Muda wa kuhudumu wa viongozi wa sasa wa ANC, akiwemo Bw Mudavadi, ulikamilika Juni 15, 2020.

Hiyo inamaanisha kuwa chama cha ANC sasa hakina viongozi.

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka sasa anatamtegemea Rais Kenyatta kujinuru kisiasa baada ya kutengwa na viongozi wengine wa maeneo ya ukambani; magavana Charity Ngilu (Kitui), Prof Kivutha Kibwana (Makueni), Alfred Mutua (Machakos) na mfadhili wa muda mrefu wa chama hicho Johnstone Muthama.

Bw Musyoka tayari ametangaza kuwa chama chake kitajiunga na Jubilee, hatua ambayo wadadisi wanasema kuwa ananuia kupata usaidizi wa Rais Kenyatta ili kurejesha ushawishi wake wa eneo la Ukambani.

  • Tags

You can share this post!

Ida Odinga azoa Sh200m katika harambee ya muda wa saa mbili

Akaunti za ‘Tangatanga’ zanyemelewa