• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:15 AM
Chelsea watakuwa moto wa kuotea mbali msimu mpya – Harry Redknapp

Chelsea watakuwa moto wa kuotea mbali msimu mpya – Harry Redknapp

Na MASHIRIKA

UKUBWA wa kiwango cha kujishughulisha kwa Chelsea katika soko la uhamisho wa wachezaji muhula huu ni onyo kwa wapinzani wao wakuu katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na soka ya bara Ulaya msimu ujao.

Haya ni kwa mujibu wa kiungo wa zamani wa kikosi hicho, Gus Poyet, 52 ambaye amesema itakuwa “aibu” na “pigo” kwa Chelsea iwapo watakamilisha kampeni za EPL msimu ujao nje ya nafasi mbili za kwanza kileleni mwa jedwali.

Mbali na Poyet, wachanganuzi wengine wa soka ya Uingereza wanahisi kwamba idadi kubwa ya wachezaji ambao Chelsea imesajili kufikia sasa inadhihirisha kiu ya kocha Frank Lampard anayepania kuanza kunyanyulia ‘The Blues’ mataji ya haiba chini ya kipindi kifupi iwezekanavyo.

“Ilivyo, ishara za Lampard ni wazi na maazimio ya Chelsea ni bayana. Kikosi hicho hakitataka masihara katika kampeni za muhula ujao wa 2020-21. Chelsea watatamba na watakuwa tishio kwa kila mpinzani,” akasema mkufunzi wa zamani wa Tottenham Hotspur, Harry Redknapp, 73.

Kufikia sasa, Chelsea wamesajili wanasoka watano wapya akiwemo beki matata mzawa wa Brazil, Thiago Silva aliyeagana na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa bila ada yoyote.

Silva, 35, alitia saini mkataba wa mwaka mmoja na Chelsea ambao watakuwa na fursa ya kurefusha zaidi kipindi cha kuhudumu kwa nyota huyo ugani Stamford Bridge kutegemea matokeo yake msimu ujao.

Aliyekuwa beki wa Nice, Malng Sarr, beki wa kushoto Ben Chilwell aliyebanduka Leicester City, fowadi Hakim Ziyech aliyetokea Ajax na mshambuliaji Timo Werner ambaye alikatiza uhusiano wake na RB Leipzig ndio wanasoka wengine waliosajiliwa na Chelsea hivi majuzi.

Hata hivyo, gazeti la Evening Standard limefichua kwamba Sarr atatumwa kwa mkopo katika mojawapo ya klabu za EPL ili ajiimarishe zaidi katika msimu wa 2020-21.

Katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Chelsea, Lampard aliyetegemea sana huduma za chipukizi, alichochea waajiri wake kumaliza kampeni za EPL katika nafasi ya nne, kutinga hatua ya 16-bora ya UEFA na kufika fainali ya Kombe la FA mnamo 2019-20.

Kikosi hicho kitakachofungua rasmi kampeni za msimu mpya wa EPL dhidi ya Brighton mnamo Septemba 14, 2020 uwanjani American Express, kinahusishwa pia na uwezekano mkubwa wa kumsajili mvamizi Kai Havertz, 21, kutoka Bayer Leverkusen nchini Ujerumani.

Lampard amefichua pia maazimio ya kujinasia huduma za kipa atakayekuwa kizibo cha Kepa Arrizabalaga anayetazamiwa kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Sevilla au Atletico Madrid.

Andre Onana wa Ajax, Jan Oblak wa Atletico na Nick Pope wa Burnley ni miongoni mwa makipa wanaoviziwa sasa na Chelsea baada ya Yann Sommer wa Borussia Monchengladbach, Dean Henderson wa Manchester United na Roman Burki wa Borussia Dortmund kutia saini mikataba mipya kambini mwa waajiri wao.

“Hali na tofauti kabisa na msimu uliopita ambapo Chelsea walipigwa marufuku ya kusajili mchezaji yeyote. Ujio wa wanasoka hawa wazoefu unawaweka mashabiki wa Chelsea katika ulazima wa kutarajia makuu kutoka kwa kikosi chao,” akasema Poyet.

“Sidhani Lampard yuko Chelsea kuwalea tu wanasoka chipukizi bila kushinda taji lolote. Kwa sasa anajivunia huduma za masogora walio na uwezo wa kutambisha kikosi vilivyo na hata kutikisa miamba wa bara Ulaya,” akaongeza.

Hata hivyo, ameitaka Chelsea kuimarisha zaidi safu yao ya ulinzi kwa kusajili beki mwingine mahiri zaidi ili kuepuka masaibu ya msimu huu wa ulioshuhudia wanafainali hao wa Kombe la FA wakifunga jumla ya mabao 54 kwenye EPL.

Hiyo ilikuwa idadi kubwa zaidi ya mabao kati ya vikosi vyote vilivyokamilisha kampeni za EPL ndani ya mduara wa 10-bora kufungwa mnamo 2019-20.

“Chelsea kwa sasa ina mseto wa chipukizi na wanasoka wazoefu wenye tajriba pevu. Hiyo itakuwa sifa itakayowafanya kuwa kivutio zaidi miongoni mwa mashabiki wa EPL,” akasema Redknapp katika mahojiano yake na Sky Sports.

“Mkurugenzi wa masuala ya spoti kambini mwa Chelsea, Marina Granovskaia ametekeleza wajibu wake. Sasa kibarua kilichosalia ni cha Lampard. Akamilishe msimu ujao katika nafasi ya pili kisha atwae taji la EPL mnamo 2021-22 bila presha yoyote,” akaongeza.

You can share this post!

Mnunuzi wa Messi sharti aweke mezani Sh89 bilioni –...

Beki Keane atia saini mkataba mpya na Everton hadi 2025