• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
ANA KWA ANA: Fundi cherehani stadi anayefumua nguo chakavu na kushona mpya zenye mwonekano wa kuvutia zaidi

ANA KWA ANA: Fundi cherehani stadi anayefumua nguo chakavu na kushona mpya zenye mwonekano wa kuvutia zaidi

Na WANGU KANURI

IDADI ya wahitimu wanaofuzu kutoka vyuo vikuu kila mwaka inazidi kuongezeka lakini nafasi za kazi zilizoko katika soko la ajira katika maeneo mengi nchini zinasalia za chini.

Hali hii imesababisha wahitimu wengi kutafuta njia mbadala za kujikimu na kujiendeleza maishani.

Isitoshe, kuzikuza talanta na ujuzi wao huku waliofaulu katika biashara zao wakiwa kioo cha walio katika vyuo vikuu somo kuu likiwa kutilia maanani suala nzima la kujitafutia njia mbadala za kupata pesa kabla ya kufuzu.

Doreen Wambui Kamemba, ni kielelezo cha wanafunzi katika vyuo vikuu kwani anajimudu kwa biashara yake ya ushonaji wa nguo.

Tueleze kwa kifupi kukuhusu

DOREEN: Doreen Wambui Kamemba ni kitindamimba katika familia ya watoto watatu wa Bw na Bi Kamemba. Nilizaliwa Julai 27, 1999. Ninasomea shahada ya Habari na Teknlojia ya Biashara katika Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kilichoko mjini Juja, Kaunti ya Kiambu.

Uligundua lini unaweza kushona?

DOREEN: Nilianza kushona nikiwa na umri wa miaka 11 ambapo nilikuwa natia lebo katika sare yangu ya shule. Halikadhalika, nilibobea katika ujuzi huu baada ya kuchagua somo la Sayansi ya Nyumbani – Home Science – nilipojiunga na shule ya upili ya wasichana ya MaryHill iliyoko Thika. Somo hilo lilinipa ari ya kujiunga na fani ya mitindo.

Wateja wako ni kina nani na wao hutaka wafanyiwe nini?

DOREEN: Asilimia 80 ya wateja wa nguo zangu huwa wasichana na kina dada rika langu huku asilimia iliyosalia ikiwa ni vijana wa kiume wa umri uo huo. Wengi hutaka nizikarabati upya nguo zao kwa fasheni mpya; hasa nguo zilizochanika au mashati walionunuliwa ama hata kujinunulia lakini yakaonekana makubwa ajabu! Hivyo basi kutokana na malighafi hayo, ninatengeneza nguo zinazovutia kimtindo.

Changamoto unazopitia katika kazi hii ni zipi?

DOREEN: Kila mteja ana mahitaji yake spesheli ambapo mimi fundi ninahitajika niwe makini zaidi kuhakikisha ninafanya kazi inayomridhisha kila mmoja. Hivyo naiona changamoto yangu kwa mtazamo chanya kuwa la muhimu zaidi katika biashara hii ni kuhakikisha wateja wangu wanafurahia kazi ya mikono yangu.

Kinachokupa msukumo wa kushona ni nini?

DOREEN: Mitindo yangu huwa ni ya ubunifu wa hali ya juu; yaani ninatengeneza nguo kutoka yanayonijia mawazoni lakini pia wakati mwingine ninapata mitindo mingine inayopendeza kutoka kwa mitandao ya kijamii ya Pinterest na YouTube.

Unajivunia nini kutokana na kazi yako?

DOREEN: Kama kila mwanabiashara kufahamu biashara yake, sawa sawa na mimi kwani nimeuelewa ufundi wa kushona kwa kutumia cherehani. Japo cherehani yangu imechakaa, ninaelewa fika kuwa kila kanyagio na tuo kwenye cherehani hiyo ndiyo chanzo cha hela zangu. Ujuzi wa kuitengeneza nguo ambayo imechakaa na kuchanika na kuiunda kwa mtindo mwingine bora, umenisaidia kuvuvia na kuwa wa kipekee katika ushoni wa nguo. Vile vile, kinachonivutia zaidi kutokana na kazi hiyo ni kutosheleza mahitaji ya wateja wangu.

Doreen Wambui Kamemba hufumua nguo chakavu na kushona mpya zenye mwonekano wa kuvutia zaidi. Picha/ Wangu Kanuri

Unatumia nyanja zipi katika kuuza bidhaa zako?

DOREEN: Kwa sasa ninatumia mitandao ya kijamii ya Instagram na pia Facebook kuuza nguo zangu. Ukurasa wangu wa Facebook na hata Instagram ni dee_revamp #Charming with Doreen. Hamna pahala popote nilipokodisha kwani mimi hushonea katika chumba changu cha malazi nyumbani kwetu lakini biashara ijapojisimamia, nitaweza kukodi pahala pa biashara.

Ugonjwa wa Covid-19 umeathiri vipi kazi yako?

DOREEN: Ugonjwa wa Covid-19 umeathiri biashara yangu kwani sina uwezo wa kupata baadhi ya majora ambayo ninahitaji katika miradi mingine. Hata hivyo, kupitia masharti yaliyotolewa na Wizara ya Afya ya kukaa nyumbani, nimeweza kuboresha uhodari wangu katika kazi hii.

Doreen Wambui Kamemba akiwa amevaa shati kubwa. Picha/ Wangu Kanuri
Doreen Wambui Kamemba akiwa na aina mpya ya nguo kutokana na shati alilofumua na kuishona yenye mwonekano wa kuvutia zaidi. Picha/ Wangu Kanuri

Una mipango gani ya siku za usoni?

DOREEN: Nitafurahi sana iwapo nitamiliki kampuni ya kutengeza aina mbalimbali za mavazi yaliyo na chapa – logo – yangu hapa nchini Kenya na katika nchi zilizoko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa kuwa ushoni ni sanaa ambayo hukaribia sana na uandishi, wewe hushona katika mazingira gani?

DOREEN: Ninaposhona, huwa ninaucheza muziki ama kusikiza podcasts sana sana. Mazingira hayo huniwezesha kubuni mitindo geni na kuifanya kazi yangu kwa ustadi mwingi.

Ungependa kuwaeleza nini wanarika wenzako?

DOREEN: Ukiwa na talanta ama ujuzi katika jambo na unapenda kulifanya jambo hilo, fuatilia lakini cha muhimu kabisa kuwa mwenye bidii katika kulifanikisha jambo hilo.

You can share this post!

Mwili wa mwanamke aliyekufa maji waendelea kusakwa

Obure na Ouko kushtakiwa kwa mauaji