Siasa

Spika wa Migori apiga ripoti polisi baada ya kutishiwa maisha

September 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Migori Boaz Okoth amesema maisha yake yamo hatarini baada ya kuvamiwa na genge la wahuni kuhusiana mchakato wa kumng’oa mamlakani Gavana Okoth Obado.

Alidai Jumamosi, Septemba 5, kwamba watu walioandamana na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, walivamia makazi yake katika mtaa wa Milimani, Kisumu Ijumaa jioni.

Amepiga ripoti kwa kituo cha polisi cha Central, jijini Kisumu, kuhusiana na kisa hicho.

Hata hivyo, Bw Sifuna alikuwa mwepesi wa kukana madai hayo akisema: “Sielewi kile anachosema. Bw Boaz Okoth aache sarakasi zisizo na maana.”

Hata hivyo, kwenye kikao na wanahabari jijini Kisumu Jumamosi, asubuhi Spika Okoth alidai Bw Sifuna aliongoza kundi na vijana katika makazi yake yaliyoko katika Ruby Court Ijumaa saa tano za usiku kwa lengo la kumdhuru.

Aliongeza kuwa mlinzi wake alijeruhiwa wakati wa shambulio hilo.

“Nilipoenda katika dari ya nyumba walikuwa wakipiga kelele na ndipo nikamwita mlinzi wangu. Alipowasili akashambuliwa. Tuko na video na nambari za usajili za magari yaliyotumiwa,” Okoth akasema.

“Kijana mmoja alimwambia mlinzi wangu kwamba wananifahamu na watakabiliana nami vilivyo,” akaongeza.

Spika Okoth alisema alitoroka kupitia lango la nyuma ya nyumba na kuelekea katika kituo cha polisi cha Central kupiga ripoti kuhusiana na shambulio hilo la usiku wa manane,” Okoth akasema.

Alisema gari fulani lilikuwa likimfuata alipokuwa akielekea katika kituo hicho cha polisi na aliporejea.

“Ni dhahiri kuwa maisha yangu yamo hatarini kuhusiana na yale ambayo yanaendelea katika kaunti ya Migori. Nimekuwa nikiugua kwa muda mrefu na sijakuwa nikiripoti kazini. Sasa mbona nitishwe na kushambuliwa?” Bw Okoth akauliza.

Spika huyo alisema kufikia Jumamosi hoja ya kumwondoa mamlakani Gavana Obado haikuwa imewasilishwa katika afisi yake lakini akaahidi kuishughulikia, kisheria, pindi itakapowasilishwa.

Mapema wiki huu, uongozi wa ODM uliwaita madiwani wa Migori Nairobi ambapo iliamuliwa kwamba gavana Obado aondolewe mamlakani kupitia hoja ya kutokuwa na imani naye.

Mkutano huo ulifanyika siku moja baada ya Gavana Obado na wanawe wawili kushtakiwa kwa wizi wa Sh73 milioni, pesa za umma kupitia utoaji zabuni katika serikali ya kaunti Migori.

Wote watatu waliachiliwa kwa dhamana ya Sh18.5 milioni pesa taslim, lakini mahakama ikaamuru Gavana Obado alifike afisini mwake hadi kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi alisema chama hicho kinataka Gavana Obado atimuliwe na Naibu wake Nelson Mahanga aapishwe kuhudumu kama Gavana hadi 2021. “Hii ndio njia ya kipekee itakayohakikisha kuwa shughuli za utoaji huduma kaunti ya Migori haiathiriwi kwa njia yoyote,” akasema Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini.