Mswada wa majina kama Hustler, Minji Minji kujadiliwa seneti
Na CHARLES WASONGA
MSWADA unaowaruhusu wanasiasa kutumia majina bandia kama majina rasmi katika karatasi za kura ni mojawapo ya miswada iliyoratibiwa kujadiliwa kuanzia Jumanne, Septemba 9, maseneta watakaporejelea vikao baada ya likizo ya mwezi mmoja.
Mswada huo ambao umedhaminiwa na Seneta wa Nyeri Ephraim Maina uliidhinishwa na Kamati ya Seneti kuhusu Sheria na Haki za Kibinadamu mnamo Agosti 25, 2020. Hatua hii inajiri mwaka mmoja baada ya kuchapishwa katika gazeti rasmi la serikali.
Ikiwa mswada huo utapitishwa kuwa sheria kiongozi wa ODM Raila Odinga atakuwa huru kutumia jina “Baba” kujitambulisha katika katika karatasi za kura ya urais.
Naye Naibu Rais William Ruto atakuwa huru kutumia jina, “Husler” huku Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru akajulikana rasmi kama “Minji Minji” atakapokuwa akitetea wadhifa wake katika uchaguzi huo utakaofanyika Agosti 9, 2022.
Mswada huo utaifanyia marekebisho Sheria ya Uchaguzi ili Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itambue majina bandia ambayo kwayo raia wanawatambua baadhi ya wanasiasa nchini; katika ulingo wa siasa.
Wakati huu, sheria hiyo ya uchaguzi inatambua tu majina rasmi yalivyo katika sajili ya wapiga kura na katika stakabadhi rasmi ambazo mgombeaji hutumia kujitambulisha, kama vile kitambulisha cha kitaifa au paspoti.
Akitetea mswada huo Seneta Maina alisema unalenga kufanikisha uchaguzi huru na haki kwa kuwawezesha wanapiga kuwachagua wale wanaowataka pasina kukanganyikiwa.
“Mswada huu pia unalinda haki ya mgombeaji ya kujieleza kwa njia huru,” akaeleza.
Hata hivyo, ilivyo sasa, mgombeaji ambaye angetaka jina lake maarufu kujumuishwa katika karatasi ya kura atalazimika kufuata utaratibu rasmi wa kubadilisha jina.
Utaratibu huo umewekwa katika Sheria ya Usajili wa Watu, Sura ya 107, Sheria ya Usajili wa Stakabadhi, Sura ya 285 na kanuni na masharti yaliyotengenezwa chini ya sheria hizo mbili.
Ikiwa mswada huo utapitishwa kuwa sheria, mgombeaji ambaye anataka jina lake maarufu litumika kumtambua rasmi katika karatasi ya kura sharti atume ombi rasmi kwa IEBC siku 21 kabla ya tarehe ya kuwasilisha majina mengine rasmi.
“Mgombeaji atawasilisha ombi kwa tume, kwa kutumia fomu rasmi ili jina lake maarufu litambuliwe rasmi,” mswada huo unasema.
Kwa mujibu wa mgombeaji huru, ombi hilo linapasa kuwasilishwa wakati ambapo atakuwa akiwasilisha alama atakayotumia uchaguzini.
Kulingana na Bw Maina sheria ya sasa ambayo inawalazimisha wagombeaji kutumia majina yao rasmi pekee hupelekea baadhi yao kukosa kura, baada ya wafuasi wao kukosa kuwatambua kwa majina yao maarufu.
“Lengo kuu la uchaguzi ni kuhakikisha kuwa wapiga kura wanawachagua viongozi wanaowataka katika mazingira huru na yenye haki. Kwa hivyo, kutambuliwa kwa jina na suala muhimu zaidi katika uchaguzi huru na wa haki na kunapasa kuendelezwa ipasavyo”
“Humwezesha mpigakura kumtambua mgombeaji anayemtaka kwa urahisi na hivyo kumpigia kura,” akasema Bw Maina aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama tawala, Jubilee.
Katika chaguzi zilizopita wanasiasa waliotaka kutumia majina yao maarufu walilazimika kutia saini hati ya kiapo ili kuweza kujumuisha majina yao “bandia” miongoni mwa majina yao rasmi katika vitambulisho vyao vya kitaifa na stakabadhi zingine rasmi.
Mifano hapa ni Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Kioko ambaye alifuata taratibu hitajika kuweza kujumuisha jina “Sonko” katika kitambulisho chake cha kitaifa.
Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu naye alifuata mkondo huo huo alipojumuisha jina “Babayao” katika majina yake rasmi.