• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Wanasoka wanne wa Liverpool kuwania taji la Mchezaji Bora wa Mwaka

Wanasoka wanne wa Liverpool kuwania taji la Mchezaji Bora wa Mwaka

Na MASHIRIKA

MASOGORA wanne wa Liverpool wamo katika orodha ya wachezaji sita ambao wameteuliwa na Chama cha Wachezaji wa Soka (PFA) kuwania taji la Mchezaji Bora wa Mwaka wa 2019-20.

Liverpool ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wanajivunia nyota Jordan Henderson, Sadio Mane, Trent Alexander-Arnold na mshindi wa taji hilo mwaka 2019, Virgil van Dijk katika orodha hiyo.

Manchester City walioambulia nafasi ya pili kwenye EPL muhula huu wanawakilishwa na kiungo Kevin de Bruyne na fowadi Raheem Sterling.

Alexander-Arnold atakuwa pia akiwania taji la Chipukizi Bora la Mwaka katika tuzo hizo zitakazotolewa kesho Jumanne ya Septemba 8, 2020.

Atatoana jasho na Tammy Abraham (Chelsea), Marcus Rashford, (Manchester United), Mason Greenwood (Manchester United), Mason Mount (Chelsea) na Bukayo Saka (Arsenal) katika kategoria hii.

Wanasoka wanne wa Chelsea – Beth England, Sophie Ingle, Guro Reiten na Ji So-yun ni miongoni mwa wale ambao wamejumuishwa katika orodha ya wawaniaji wa taji hilo kwa upande wa wanawake.

Mshindi wa mwaka jana, Vivianne Miedema na mwenzake wa kikosi cha Arsenal, Kim Little wanaikamilisha orodha hiyo.

Wakati uo huo, Everton wamethibitisha kumsajili kiungo matata mzawa wa Brazil, Allan Marques Loureiro, 29, ambaye amekatiza rasmi uhusiano wake na Napoli kwa kima cha Sh3 bilioni.

Anakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na kocha Carlo Ancelotti aliyewahi kumtia makali kambini mwa Napoli, Italia.

Everton pia wako pua na mdomo kujinasia huduma za Abdoulaye Doucoure kutoka Watford na James Rodriguez wa Real Madrid. Kikosi cha Ancelotti kimeratibiwa kufungua kampeni za msimu mpya wa EPL dhidi ya Tottenham Hotspur ugenini mnamo Septemba 13, 2020.

Arsenal pia wamethibitisha kumsajili kiungo Dani Ceballos, 24, ambaye amejiunga nao upya kutoka Real kwa mkopo wa mwaka mmoja zaidi.

Nyota huyo mzawa wa Uhispania aliyejiunga na Madrid kutoka Real Betis mnamo 2017, alichezea Arsenal jumla ya mechi 37 msimu huu wa 2019-20. Alifunga bao la ushindi katika robo-fainali za Kombe la FA dhidi ya Sheffield United na akawa sehemu ya kikosi kilichowabwaga Chelsea kwenye fainali na kutwaa taji hilo kwa mara ya 14 mnamo Agosti 1, 2020.

Chelsea pia wamejinasia maarifa ya kiungo Kai Havertz ambaye ameagana rasmi na Bayer Leverkusen ya Ujerumani kwa kima cha Sh9.9 bilioni.

Sogora huyo amerasimisha uhamisho wake kwa mkataba wa miaka mitano. Ndiye mwanasoka ghali zaidi kuwahi kusajiliwa na Chelsea baada ya kipa Kepa Arrizabalaga aliyeondoka kambini mwa Athletic Bilbao kwa Sh10 bilioni mnamo 2018.

Katika msimu wa 2019-20, Havertz alifunga mabao 36 na kuchangia mengine 25 katika jumla ya mechi 118 alizowachezea Leverkusen.

You can share this post!

FKF yatoa ratiba ya uhamisho wa wachezaji katika ligi ndogo

Maseneta sasa waamua kuharakisha mswada wa kuwezesha kaunti...